Msijaribu 'surgery' kuongeza makalio, iliniathiri! - Muna Love

Muhtasari

• Muna Love anazidi kulilia mateso ya upasuaji wa kuongeza makalio alioufanya ambao ulimuendea mrama, awashauri wanadada wasijaribu.

Muna Love
Image: Instagram

Muigizai na mwanamitindo Muna Love ametoa ushauri kwa wanadada wanaodhamiria kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha muonekano wa miili yao na kuwaambia katu wasiwaze kitu kama hicho kwani yeye alijaribu na kimemuathiri kwa asilimia kubwa mwilini mwake.

Mwanadada huyo ambaye kama mwezi mmoja hivi uliopita alitangaza kufanyiwa upasuaji ili kuongeza makalio na ‘dimples’, upasuaji ambao ulimuendea mrama kwa kuumwa mno mpaka akatangaza kurudi kwa Mungu kwa kusali aliandika kwenye instastories zake wikendi iliyopita akitolea ushauri kwa wanadada wasijaribu upasuaji wa aina hiyo.

Baada ya kusema ameanza kupata nafuu, Muna aliwataka wafuasi wake kuwa na subra kwa sababu angeweka wazi kila kitu mpaka kusema kidonda ambacho kilikuwa kinauma sana lakini amekaa kimya tangu muda huo na mashabiki wake hawaonekani kukimya kwani wamemkumbusha kwamba ahadi ni deni naye akaamua kujibu japo kwa muhutasari.

“Mimi nililia na Mungu na nilisema nitasema ukweli wote na ushuhuda wa picha na kidonda change pia na maeneo mengine yalivyoathirika. Na pia naishi na madhara na siwezi kurudia makosa. Nimeumwa, mmenichamba na ningekuwa sina msaada ningekufa kwa maneno, maana nilikuwa najiangalia ninavyochambwa nasema Mungu niokoe. Ila naogopa kuongea maneno na mkae mkijua kwamba nikiwaambia madhara ambayo mimi ninayo wala sifichi ila kila surgery ina madhara yake. Nitakuja kuongea mwanzo hadi hatua ya mwisho. Ngojeeni kwanza nipumue.” Aliandika Muna kwenye instastories zake.

Pia amesema anapotoa ushauri wa madhara ya upasuaji huo hamaanishi kumzuia mtu kuitafuta ila kama kuna mwenye anabisha ako tayari aende tu bali ametahadharisha kwamba atakayekaidi atakuja kumkumbuka.

“Na sijamuia mtu kuenda kwa ajili ya upasuaji huu, nenda na utakuja kunikumbuka. Hata ushuhuda wa moyoni mimi ni mhanga na nitawajuza tu,” aliandika Muna Love.

Pia alisisitiza kwamba wanadada wasiendee upasuaji wa aina hiyo kwani kuna kule kuirudia na kama huna pesa basi kitakuwa kilima cha kukwea na hapo ndio hata madhara yatazidi mara dufu.