Muigizaji Dennis Mugo 'OJ' afunguka jinsi mamake alivyomsaidia kupambana na uraibu wa pombe

Muhtasari

•Mwigizaji huyo alieleza kuwa alikuwa amethiriwa sana na uraibu wa pombe kiasi cha kwamba hangeweza kufanya kazi bila kubugia mvinyo.

•Alifichua kuwa mama yake na mwigizaji mwenzake Ashley Murugi ndio walimsaidia kuweza kusimama tena baada ya uraibu wa pombe kuathiri taaluma na mahusiano yake.

Image: INSTAGRAM// DENNIS MUGO OJ

Mwigizaji mashuhuri Dennis Mugo almaarufu kama OJ kutokana na kipindi 'Tahidi High' amekiri kuwa amekuwa akipambana na uraibu wa pombe kwa muda mrefu.

Akiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, OJ ambaye kwa sasa anafanya kazi na serikali ya kaunti ya Embu alisema kuwa umaarufu mkubwa ambao alipata kutokana na uigizaji wake ulimfanya achanganyikiwe hadi akazama kwenye uraibu wa pombe.

Mwigizaji huyo alieleza kuwa alikuwa amethiriwa vibaya na uraibu wa pombe kiasi cha kwamba hangeweza kufanya kazi bila kubugia mvinyo.

"Lazima ningeamka asubuhi nipige kitu ndio nijiskie mbunifu zaidi. Nilikuwa nimeamini kuwa singefanya kazi bila pombe.Lazima ningepiga kitu ili niweze kubuni mistari ama nijue jinsi tungepiga picha. Ilifika hatua hiyo na iliniathiri sana taaluma yangu," Mugo alisema.

Mugo alisema safari ya kukwamka kutoka kwa uraibu wa pombe haijakuwa rahisi kwake kwani imekumbwa na changamoto si haba.

Mwigizaji huyo alifichua kuwa mama yake na mwigizaji mwenzake Ashley Murugi ndio walimsaidia kuweza kusimama tena baada ya uraibu wa pombe kuathiri taaluma na mahusiano yake.

"Mama alikuwa wa kwanza kugundua kuwa nimeathirika. Alisema kuwa sikuwa naendelea vizuri. Alipendekeza niende rehab. Kuenda rehab nikacheki wasee wenye wako huko nikaona bado sijafika hapo.  Wakati huo nilikuwa nimeachana na baby mama. Nilikuwa nishapata mtoto na ulevi uliathiri uhusiano wangu na mamake. Mambo yalikuwa yameharibika. Mama  alinichukua miezi mitatu akitaka kujua  kama niko pabaya kama alivyodhani," Mugo alisema.

Mwigizaji huyo amemshukuru mamake pamoja na Ashley kwa kumsaidia wakati mambo yote yalikuwa yanamharibikia.

Kwa sasa Mugo anafanya kazi katika sekta ya sanaa na burudani ya kaunti yake ya nyumbani, Embu.