Ugali Man afunguka jinsi umaarufu uliokoa ndoa yake

Muhtasari

•Baba huyo wa watoto watatu  alieleza kuwa mikwaruzano ilipungua katika ndoa yake kwani aliweza kukimu mahitaji ya familia.

•Pia  alifichua kuwa baada ya kupata umaarufu na kupata manufaa  makubwa ya kifedha alizamia kwenye biashara huku akifungua Gym ya kisasa maeneo ya Ongata Rongai.

Charles Odongo almaarufu kama 'Ugali man'
Charles Odongo almaarufu kama 'Ugali man'
Image: Hisani

Mtaalamu wa mazoezi Charles Odongo almaarufu 'Ugali Man' amefunguka jinsi umaarufu mkubwa aliopata mwaka jana ulimbadilishia maisha.

Akiwa kwenye mahojiano na Tuko Extra, Odongo alisema kuwa manufaa yaliyokuja na umaarufu yalileta utulivu katika ndoa yake.

Baba huyo wa watoto watatu  alieleza kuwa mikwaruzano ilipungua katika ndoa yake kwani aliweza kukimu mahitaji ya familia.

"Malumbano ya nyumbani yamepungua kabisa. Shida za kifedha huchangia katika mikwaruzano mingi ya kinyumbani. Lakini angalau mkiwa mmejipanga mnapata hakuna shida. Mikwaruzano hiyo inapunguka tena kabisa  zaidi kwa kuwa mamaa anapata chenye anataka na anaishi vizuri. Watoto pia wako fiti na wanakula poa," Odongo alisema.

Mtaalamu huyo wa mazoezi ambaye alipata umaarufu mkubwa kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kula ugali alifichua kuwa mke wake ni mzaliwa wa Uganda. Alisema wamebarikiwa na mabinti wawili na mvulana mmoja pamoja.

Odongo pia  alifichua kuwa baada ya kupata umaarufu na kupata manufaa  makubwa ya kifedha alizamia kwenye biashara huku akifungua Gym ya kisasa maeneo ya Ongata Rongai.