Nadia Mukami na Arrow Bwoy wazindua wakfu kwa heshima ya mtoto waliyepoteza

Muhtasari

•Nadia alisema Lola & Safari Foundation italenga wasichana wadogo na kina mama ambao hukabiliwa na changamoto katika kipindi cha ujauzito.

•Mwanamuziki huyo alisema kwamba alipata wazo hilo baada yaujauzito wake wa kwanza kuharibika mwaka jana.

Nadia Mukami na Arrow Buoy katika hafla ya uzinduzi wa Lola and Safari Foundation
Nadia Mukami na Arrow Buoy katika hafla ya uzinduzi wa Lola and Safari Foundation
Image: KALONDU MUSYIMI

Wanandoa mashuhuri Nadia Mukami na Arrow Bwoy wamezindua wakfu mpya kwa jina Lola & Safari Foundation.

Akihutubia wanahabari katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Jumanne, Nadia alisema Lola & Safari Foundation italenga wasichana wadogo na kina mama ambao hukabiliwa na changamoto katika kipindi cha ujauzito.

Malkia huyo wa muziki alisema walipatia wakfu huo jina 'Lola & Safari' kwa heshima ya mtoto wao ambaye alikufa tumboni kabla ya kuzaliwa.

"Lola & Safari ni jina ambalo tulikusudia kupatia mtoto wetu lakini hatukufika hapo. Sihitaji kulizungumzia kwa sasa. Ni wakfu muhimu sana kwetu. Ni kitu kizuri hapa. Katika Lola & Safari Foundation tutasaidia, kuelimisha na kushauri wasichana na kina mama wadogo," Nadia alisema.

Mwanamuziki huyo alisema kwamba alipata wazo hilo baada yaujauzito wake wa kwanza kuharibika mwaka jana. 

Alisema matatizo ambayo alishuhudia wakati wa ujauzito wake yalimsukuma kutafuta washirika ili kuanzisha mradi huo.

"Lola & Safari ya Nadia Mukami na Arrow Bwoy ni Wakfu unaolenga wasichana na akina mama wadogo ambao wanapitia changamoto za ujauzito, kuzaa, unyogovu baada ya kuzaa na wale ambao hawawezi kumudu huduma za afya ya uzazi na pia kuja na mpango sahihi wa kifedha. Lola na Safari Foundation pia inaangazia wasichana matineja ambao wameacha shule kwa sababu ya mimba za utotonina inatoa uhamasishaji kwa wasichana wachanga juu ya ujauzito," Nadia alisema.

Wanandoa hao walisema watakuwa wanafanya tamasha za hisani, kutembelea mitaa ya mabanda na kufanya michango katika juhudi za kufanikisha ndoto yao ya kusaidia wanawake katika safari zao za ujauzito.