"Mama alinitupa baada ya kunizaa, baba alikufa kabla nimuone," Ringtone afunguka kuhusu utoto wake mgumu

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alifichua kuwa kabla ya kuwa chokora alilelewa na nyanyake baada ya mamake kumtupa na babake kumkataa.

•Baada ya kumpoteza nyanyake, Ringtone alizamia maisha ya mitaani kwa kuwa hakuwa na kwingine kwa kuenda.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko amefunguka kuhusu jinsi alivyojipata mitaani kama chokoraa katika siku zake za utotoni.

Akiwa kwenye mazungumzo na Diana Marua, Ringtone alifichua kuwa hakupata fursa ya kulelewa na wazazi wake kwani wote wawili walijitenga naye akiwa mchanga sana.

Mwanamuziki huyo alifichua kuwa kabla ya kuwa chokora alilelewa na nyanyake baada ya mamake kumtupa na babake kumkataa. Alieleza kuwa alipambana na mengi magumu akiwa kwa nyanyake.

"Babangu alikuwa mlevi wakakosana na mamangu. Mama aliponizaa aliniweka kwa kijisanduku akaenda akaniacha nje ya baa ambapo babangu alipenda  kulewa. Baba hakuwa pale lakini ndugu yake ambaye alikuwa anauza nguo Tom Mboya Street alikuwepo. Niliokotwa nikaenda kuishi na nyanyangu. Nilikua nikiwa na Kwashiakor, nywele yangu illikuwa nyekundu. Nililelewa na nyanyangu. Baba alikufa nikiwa na miaka mitano. Nyanya akafa nikiwa na miaka saba. Wakati ambao niliona babangu ni akizikwa, ata sikuingia kwa kuwa sikuwa na uhusiano. Nyanyangu alikuwa baba na mama yangu," Ringtone alisimulia.

Ringtone alisema alilia sana wakati nyanya yake alifariki kwa kuwa ndiye pekee alikuwa amechukua nafasi ya wazazi wake wasiokuwepo.

Baada ya kumpoteza nyanyake, Ringtone alizamia maisha ya mitaani kwa kuwa hakuwa na kwingine kwa kuenda.

"Wakati nyanyangu alikufa ndio nililia kabisa nikamaliza. Nililia sana. Alikuwa kila kitu kwangu. Baada ya hapo nilienda nikawa chokoraa," Alisema.

Mwanamuziki huyo alifichua kuwa alipokuwa mitaani alikuwa na ndoto kubwa, nyingi ambazo ameweza kutimiza kufikia sasa.