"Mimi najitafutia mwenyewe!" Esma Platnumz azungumzia pesa za kakake Diamond Platnumz

Muhtasari

•Esma aliweka wazi kuwa huwa anatia bidii kujitafutia pesa zake mwenyewe na nduguye Diamond vilevile anajitafutia pamoja na familia yake.

•Mfanyibiashara huyo aliwashauri wanawake wengine kuamka na kutia bidii kazini ili kuweza kujitegemea wenyewe.

Esma Platnumz na Diamond Platnumz
Esma Platnumz na Diamond Platnumz
Image: HISANI

Mfanyibiashara Esma Platnumz ameweka wazi kuwa hategemei pesa za kakake mdogo Diamond Platnumz kukidhi mahitaji yake na familia yake.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media,  mama huyo wa watoto wawili alisema  kamwe hajawahi kubali  kujibweteka eti kwa kuwa kakake ni tajiri mkubwa.

Esma aliweka wazi kuwa huwa anatia bidii kujitafutia pesa zake mwenyewe na nduguye Diamond vilevile anajitafutia pamoja na familia yake.

"Ulimwengu wa sasa hivi huwezi kumtegemea kakako, babako  ama nduguyo yeyote. Unatakiwa kama mwanamke usimame mwenyewe. Mimi nina watoto na wananiangalia. Mtoto wangu atachukuaje mfano kutoka kwangu. Atasema alale jinsi mamake alivyolala??  Hata watoto wangu nikikaa nao huwa nawapa mifano. Huwa nawaambia wasikae wajibweteke kwa kuwa mjomba wao ana pesa, hapana. Mimi najitafutia pesa kwa ajili ya watoto wangu naye Naseeb anajitafutia pesa kwa ajili ya familia yake. Ni vitu viwili tofdauti," Esma alisema.

Mfanyibiashara huyo aliwashauri wanawake wengine kuamka na kutia bidii kazini ili kuweza kujitegemea wenyewe.

"Wanawake wenzangu tusibweteke. Katika dunia ya sasa hivi, hata huyo mwanaume hataki mwamke ambaye hafanyi kazi," Esma alisema.

Esma ni miongoni mwa wanawake maalum ambao Diamond Platnumz alisherehekea mnamo siku ya wanawake duniani iliyoadhimishwa hivi majuzi.