'Walipelekwa ICU ndani ya karatasi za nailoni,' Isaac Mwaura afunguka kuhusu kiwewe cha kupoteza wanawe

Muhtasari

• Mwaura alisema mnamo Januari 2017 mkewe alijifungua watoto watatu kabla ya wakati,  wavulana wawili na msichana mmoja.

• Bintiye wa pekee ndiye alitangulia kufariki baada ya siku mbili tu huku mvulana mmoja akifariki siku chache baadae.

•Mwaura alisema familia yake ilikaa hospitalini kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili na kufikia wakati wa kutoka bili ilikuwa imepanda hadi Sh 11.2M.

Nelius Mukami na Isaac Mwaura
Nelius Mukami na Isaac Mwaura
Image: INSTAGRAM

Seneta mteule Isaac Mwaura amefunguka kuhusu kiwewe cha kuwapoteza watoto wake wawili  siku chache tu baada ya kuzaliwa.

Akiwa kwenye mahojiano na Ala C, Mwaura alisema mnamo Januari 2017 mkewe alijifungua watoto watatu kabla ya wakati,  wavulana wawili na msichana mmoja. Wakati huo kampeni zake za kuwania kiti cha ubunge cha Ruiru zilikuwa zimechacha.

"Tulikuwa tunachangisha pesa za kufanya usajili mkubwa wa wapiga kura wa Kiambu. Nikipigiwa simu mwendo wa saa nne usiku nikaambiwa mke wangu anaugua. Niliambia dereva ampeleke hospitali kwa kuwa sikuwepo. Kutokana na presha za kampeni sikuweza kuenda pale usiku huo. Asubuhi nilipokuwa najiandaa kutoka nikapigia mke wangu simu akaniambia kuwa anapelekwa katika chumba cha upasuaji ili kujifungua watoto," Mwaura alisimulia.

Mwanasiasa huyo alifichua kuwa alipofika hospitalini alipata vijitoto vitatu vidogo mno vikipelekwa ICU vikiwa vimewekwa ndani karatasi za nailoni. Bintiye wa pekee ndiye alitangulia kufariki baada ya siku mbili tu huku mvulana mmoja akifariki siku chache baadae.

Mwaura alisema familia yake ilikaa hospitalini kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili na kufikia wakati wa kutoka bili ilikuwa imepanda hadi Sh 11.2M.

"Nilipata watoto wadogo sana. Walikuwa wamekaa tumboni wiki 28 pekee. Walikuwa wamewekwa ndani ya karatasi za nailoni wakitolewa wodi ya uzazi kupelekwa ICU ya watoto. Hata sikuruhusiwa kuwaona. Mamangu alikuwa anasherehekea kuwa amezaliwa. Baada ya siku mbili, msichana akafariki. Alikuwa anaitwa Njeri. Nilimpenda sana kwa kuwa yeye ndiye alikuwa msichana pekee. Alifanana sana na mke wangu. Tulikaa hospitali siku 72 ambazo zilifuata. Mwanangu Mwaura Jnr aliamshwa mara 20, pia naye akafariki. Tulipitia jehanamu na tukawa na bili ya milioni 11.2.

Siku moja baada ya mke wangu kujifungua hata mimi nililazwa hospitalini kwa kuwa nilikuwa nafanyiwa upasuaji mdogo. Kwa wakati huo sote watano tulikuwa tumelazwa Nairobi hospital. Baada ya hapo tulipatwa na kiwewe kikubwa," Mwaura alisema.

Mwanasiasa huyo alisema familia yake ilipitia kipindi kigumu baada ya kupoteza watoto hao wawili. Alisema mkewe alikumbwa na msongo wa mawazo kwa kipindi kirefu kutokana na tukio hilo la kutisha.