Seneta Isaac Mwaura akumbuka changamoto za kukua bila babake

Muhtasari

•Mwaura alifichua kuwa alikumbana na changamoto mbalimbali za kimaisha baada ya babake kumkana punde baada ya kuzaliwa.

•Mwanasiasa huyo alifichua kuwa alikataa kutumia jina la mamake na akaamua kujitambulisha kwa jina la babu yake. 

Seneta Mteule Isaac Mwaura
Seneta Mteule Isaac Mwaura
Image: MAKTABA

Seneta mteule Isaac Mwaura amesema kuwa hakuna mtoto anayestahili kukua bila uwepo wa babake mzazi.

Akiwa kwenye mahojiano na Ala C, Mwaura alifichua kuwa alikumbana na changamoto mbalimbali za kimaisha baada ya babake kumkana punde baada ya kuzaliwa.

Mwaura ambaye alikataliwa na babake akiwa mchanga kutokana na hali yake ya uzeruzeru alisema kumkosa mzazi huyo wake maishani kulimfanya akose ujasiri.

"Sauti ya mwanaume hupatia mtu ujasiri. Wakati mtu anapoenda shuleni kisha aulizwe jina la mzazi kisha aseme la mamake angeulizwa babake ako wapi. Watu wakizungumzia baba zao singeweza kusema chochote kwa kuwa sikuwa na baba. Ujasiri huwa unashuka. Unaona kama kwamba hustahili," Mwaura alisema.

Mwanasiasa huyo alifichua kuwa alikataa kutumia jina la mamake na akaamua kujitambulisha kwa jina la babu yake. 

Mwaura alifichua kuwa babake alijitenga naye punde baada yake kuzaliwa takriban miongo minne iliyopita. Alisema babake hakuridhishwa na maumbile yake na kuibua madai kuwa hakuna uwezekano wa mtoto kama yeye kutoka kwa familia yao.

"Nyumbani kwetu asili  ni Githunguri. Hata hivyo nimelelewa Githurai. Mama alikuwa anafanya kazi ya kuunda chaki kwa kampuni iliyokuwa Ruiru. Baba aliponiona alisema kwao hakuzaliwi watoto wanaofanana na Mwaura. Mimi ni mtoto wa mama single ," Mwaura alisimulia.

Mgombeaji huyo wa ubunge wa Ruiru katika uchaguzi wa Agosti alieleza kuwa mamake alichukua majukumu yote ya malezi baada ya babake kuwatoroka.