"Nitaendelea kuishi kwa upendo kamili na ukarimu" Betty Kyalo asherehekea kutimiza miaka 33

Muhtasari

•Betty amesema kuwa ataendelea kuonyesha upendo, ukarimu na kuwajali watu wote wanaohusiana naye.

•Mama wa binti mmoja pis amesema kuwa anastahili furaha na mambo yote mazuri kwa sababu ameyachuma.

Image: INSTAGRAM// BETTY KYALLO

Hivi leo, Machi 15, Mtangazaji na mfanyibiashara mashuhuri Betty Kyalo anaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake.

Mtangazaji huyo ambaye aliwahi kuhudumu katika vituo mbalimbali vya runinga nchini Kenya anatimiza miaka 33.

Akisherehekea siku hiyo maalum kwake, Betty amesema kuwa ataendelea kuonyesha upendo, ukarimu na kuwajali watu wote wanaohusiana naye. Ameapa kutokubali kushinikizwa kubadili mwelekeo wa maisha yake.

"Nitaendelea kuishi maisha kwa upendo na fadhili kabisa. Nitaendelea kuwajali watu walio karibu nami na nitatoa mkono wa usaidizi pale ambapo nina uwezo wa kushawishi hali. Ulimwengu hautanigeuza kamwe kwa kitu kingine chochote isipokuwa mwanamke mzuri, mpole na mwenye nguvu. #33," Betty amesema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama wa binti mmoja pia amesema kuwa anastahili furaha na mambo yote mazuri kwa sababu ameyachuma.

Mamia ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri wameendelea kumtakia mtangazaji huyo kheri za siku ya kuzaliwa.