'Diamond si mgeni wa sheria na kanuni za BASATA'

Muhtasari

•Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo Diamond alidai kuwa hawezi kuondoka nchini humo kwa uhuru kama wasanii wengine.

•Bwana Matiko amesema huenda watu wamemnukuu vibaya Diamond maana mwanamuzi huyo anafahamu sheria na utaratibu uliopo nchini Tanzania

Diamondplatnumz
Diamondplatnumz
Image: Instagram KWA HISANI

Wiki hii, vyombo vya habari viliandika kuhusu Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania, Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz akiilalamikia serikali ya Tanzania kumchukulia kama mhalifu anapotaka kusafiri nje ya nchi licha ya kuwa yeye ni miongoni mwa walipakodi wakubwa katika tasnia ya burudani nchini humo.

Msanii huyo ambaye kwa sasa yuko kwenye ziara ya vyombo vya habari nchini mwake kutangaza albamu yake mpya ya kidigitali- EP, inayoitwa FOA , anadai wasanii walio chini ya lebo yake ya Wasafi record wamekuwa wakifedheheshwa na kutendewa ndivyo sivyo na serikali.

Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo Diamond alidai kuwa hawezi kuondoka nchini humo kwa uhuru kama wasanii wengine.

Hata anaposafiri katika shughuli za kibinafsi kama kwenda kuwaona watoto wake wawili wanaoishi Afrika Kusini, lazima apate kibali.

Ili kupata ufafanuzi wa madai haya Mwanahabari wetu Anne Ngugi amezungumza na Matiko Muniko- Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania- BASATA .

Bwana Matiko amesema huenda watu wamemnukuu vibaya Diamond maana mwanamuzi huyo anafahamu sheria na utaratibu uliopo nchini Tanzania na yeye pamoja na lebo yake ya Wasafi wanafuata kanuni zote likija suala la kutoka nje ya nchi.

"Kwa upande wa wasanii, huu ni utaratibu wa kawaida ambao kila msanii huwa anauchukua, vibali vya wasanii wanaochukua kwa ajili ya sanaa."

Katibu huyo aliongeza kusema kuwa wao wanashughulika na watu wanaoshughulika na sanaa, hivyo kama mtu ana safari zake nyingine ambazo si za sanaa basi hahitaji kibali kutoka kwao.

Kila nchi huwa ina viza, kama hiyo nchi umeandika shughuli zako ni sanaa basi wao ndio wanapohusika lakini kama sivyo basi maelezo kwa mamlaka yatakuwa tofauti.

Ili wasanii kupata elimu ya jinsi baraza la sanaa linafanya kazi huwa tunatoa elimu katika majukwaa mbalimbali kuhakikisha kuwa wadau wetu wanapata elimu.