Diamond, wasanii watoa sababu za kupinga uteuzi wa Steve Nyerere

Muhtasari

• Wasanii wamesema kwamba yeye sio mwanamuziki na hivyo hapaswi kushikilia nafasi hiyo.

• Diamond Platnumz alisema kwamba hatua hiyo ni ya kuikosea heshima sekta ya burudani.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Wanamuziki mbalimbali kutoka Tanzania wamesuta vikali uteuzi wa Steve Nyerere kama msimamizi wa muungano wa wasanii.

Kupitia jumbe walizoachia katika kurasa zao za Instagram, wanamuziki hao walionyesha kukasirika kwao kwa kile wanachokitaja kwamba Nyerere hajawahi kuimba na hivyo hana vigezo vyovyote vya kuwaongoza.

Ifahamike kwamba Steve Nyerere amekuwa akijihusisha sana na filamu, huku hatua yake kuteuliwa kusimamia wanamuziki ikizidi kuibua hisia changamano miongoni mwa mashabiki, wasanii na washikadau mbalimbali wa burudani.

"Nina mapenzi mengi na heshima kwa ndugu yangu Steve Nyerere, tunaheshimiana na siku zote amenisapoti kwenye mambo mbalimbali. Kuna mambo mengine anaweza kufanya kujenga taifa, msilazimishe kumweka sehemu ambayo mnajua kabisa si sahihi," Diamond Platnumz aliandika.

"Naomba kujua mmetumia vigezo vipi? Kina nani kamchagua?" Nay Wa Mitego aliandika.

Aidha kuna baadhi ambao walipongeza uteuzi huo wakisema Nyerer anapaswa kupewa muda ili kutimiza majukumu yake.

"...Mngehudhuria vikao vya maamuzi, nasimama na Stive Nyerere," aliandika Mwijaku.

"Maoni yenu tumeyaona na kuyazingatia. kwa ufupi tumeziona pande zote tatu za hisia, wapo wanaoamini anafaa, wapo wanaoamini hafi , wapo ambao wanataka kujua atafanya nini akipewa muda. Tunaomba muwe na subira kesho shirikisho litatoa tamko," Fid Q aliandika.

Kulingana na Diamond Platnumz ni kwamba kwa sasa muziki wa Bongo unahitaji kusimamiwa na mtu ambaye ana uelewa na anaweza kuupeleka katika viwango vya kimataifa.

Aliongezea kwamba muziki una mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa na hivyo basi hupaswi kuchukuliwa poa tu.