Nimewahi kuvunjwa moyo mara nyingi- Zari Hassan akiri

Muhtasari

•Zari Hassan na mpenzi wake wa zamani Diamond Platnumz kutoka Tanzania wanawakilisha Kanda la Afrika Mashariki katika ya 'Young, Famous and African'.

•Amekiri kuwa amekabiliana na changamoto nyingi maishani na amewahi kuvunjwa moyo mara nyingi.

Hivi leo, (Machi18, 2021)  Netflix inatarajiwa kuachia Reality Show 'Young, Famous and African' ambayo imesubiriwa kwa hamu na ghamu.

Shoo hiyo inashirikisha baadhi ya wasanii wa Afrika wenye umri usio mkubwa, matajiri na ambao wana ufuasi mkubwa. Itaangazia maisha ya kila siku ya wasanii hao na watakuwa wanazungumzia mambo mbalimbali kuwahusu.

Mwanasoshalaiti na mwanabiashara maarufu kutoka Uganda, Zari Hassan na mpenzi wake wa zamani Diamond Platnumz kutoka Tanzania wanawakilisha Kanda la Afrika Mashariki katika shoo hiyo.

Katika kipande kifupi cha shoo hiyo ambacho alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, Zari anasikika akitoa maelezo machache kuhusu maisha yake.

"Jina langu ni Zarina. Niite Zari the Boss Lady. Mimi ni Boss Lady anayefanya kazi kwa bidii na napata kila kitu nitakacho kwa sababu nafanya kazi kwa bidii," Zari anajitambulisha katika video hiyo.

Mama huyo wa watoto watano anaendelea kutoa historia fupi kuhusu familia na mahusiano yake ya awali. Anakiri kuwa amekumbana na changamoto nyingi maishani na amewahi kuvunjwa moyo mara nyingi.

"Mimi ni mama wa watoto watano. Watatu nilipata na mpenzi wangu wa zamani na wawili wadogo nilipata na Diamond. Nimevunjwa moyo mara nyingi na nimekabiliana na changamoto nyingi, lakini huwa napambana kila wakati," Zari anasikika akisema.

Pia anazungumzia uhusiano na Diamond wa sasa huku akiweka wazi kuwa wao ni marafiki wakubwa wasio na kinyongo kwa mwingine.