Harmonize awapa msaada watu 1000 wenye mahitaji maalum

Muhtasari

•.Kando na kuwaburudisha, Harmonize pia aliwaandalia watu hao chakula na vinywaji. Vilevile aliwapa msaada wa kifedha.

•Alisema kuwa anatumai kuwa kila mwaka ataweza kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na makundi hayo.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Siku ya Jumapili staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize aliandaa tamasha ya hisani kwa watu wenye mahitaji maalum.

Tamasha hiyo ambayo iliandaliwa Mlimani City ilihudhuriwa na takriban watu 1000 wenye mahitaji maalum wakiwemo mayatima, wajane na wasio na makazi.

Akizungumza na wanahabari, Harmonize alisema lengo la tamasha hilo la 'One Love' ni kuleta furaha kwa makundi ya watu wenye mahitaji.

"Lengo ni kuona kwa kiasi kigani tunaweza kutengeneza faraja kwa kila mtu  hasa kwa makundi ya watu wenye  wanahitaji kupata faraja kutoka kwa sisi ambao tunapata riziki kwa urahisi. Lengo ni kusaidia watu ambao wanapitia wakati mgumu  kupata vitu hivyo," Harmonize alisema.

Harmonize alisema aliamua kutumia fursa ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa kuburudika na watu wenye mahitaji.

Kando na kuwaburudisha, Harmonize pia aliwaandalia watu hao chakula na vinywaji kochokocho. Vilevile aliwapa msaada wa kifedha. Alisema kuwa anatumai kuwa kila mwaka ataweza kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na makundi hayo.

"Panapo majaliwa ya Mwenyezi Mungu tutakuwa na mwendelezo huo. Kama tutajaliwa riziki, Inshallah," Alisema.

Pia alihimiza watu wengine hasa wassanii kujitolea kuleta furaha kwa makundi hayo yenye mahitaji maalum.

Harmonize alisherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Machi 15.