Khadija Kopa: Zuchu na Diamond kama wanapendana, wataoana tu

Muhtasari

• Kwani Diamond ni mwanamke au mwanaume? Mtu yeyote akija bora ni mwanaume na bora wamependana wenyewe wataoana tu wala hamna tabu - Khadija Kopa.

Malkia wa mipashi na taarab, Khadija Kopa
Malkia wa mipashi na taarab, Khadija Kopa
Image: INSTAGRAM

Malkia wa muziki wa Taarab nchini Tanzania, Khadija Kopa ambaye pia ni mamake na Zuchu ametema nyongo kuhusu ishu nzima inayohusisha familia yake na familia ya kina Diamond kupitia mwanawe Zuchu kuwepo pale Wasafi.

Akizungumza katika mahojiano na runinga moja nchini humo, Khadija Kopa aliweka wazi kwamba maneno yanayosambazwa mitandaoni eti ana ugomvi na mamake Diamond ni uongo tu wa wafitinishaji.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na maneno kwamba mamake Diamond Platnumz ana ugomvi wa chinichini na Khadija Kopa na hataki suala lolote linalowahusisha Diamond na Zuchu katika mahusiano ya kimapenzi.

Kopa amesema kwamab yeye tokea zamani hajawahi kuwa na ukaribu na mama Diamond na kusema kwamba hilo halimaanishi wao ni maadui kwani huwa wanakutana katika shughuli mbalimbali, wanacheka na kufurahi lakini hawana urafiki wa karibu vile.

Alipoulizwa kuhusu mchongo mzima wa mahusiano kati ya mwanawe Zuchu na msanii Diamond, Khadija Kopa alionekana kushikwa na kigugumizi na hatimaye kupata pumzi ambapo alikwepa suala hilo kwa kusema kwamba hangetaka kulizungumzia. Alisema kwamba amechagua kukaa kimya kwa hilo kwa sababu hangetaka kuwapa wenye midomo mada ya kuhanikiza katika mitandao ya kijamii.

Pia alisema kwamba iwapo Diamond atapeleka posa rasmi ya kumuoa Zuchu, yeye na familia nzima hawatakuwa na kizingiti chochote kwani ndoa ni kheri ambayo kila mzazi anamtakia mwanawe.

“Kwani Diamond ni mwanamke au mwanaume? Mtu yeyote akija bora ni mwanaume na bora wamependana wenyewe wataoana tu wala hamna tabu.” Alijibu Kopa alipoulizwa kuhusu uwezekano wa ndoa ya Zuchu na Diamond.