Nyerere aitaka BASATA na Wasafi kutatua tofauti zao

Muhtasari

• Msemaji na mratibu wa shughuli za sanaa katika shirikisho la sanaa Tanzania amelitaka baraza la sanaa, BASATA kutafuta njia mwafaka ya kumaliza tofauti zao na rekodi lebo ya Wasafi kwa ajili ya kujali maslahi ya wasanii.

• Ameyasema haya baada ya BASATA kutoa orodha ya wasanii watakaowania tuzo za Tanzania Music Awards ambapo wasanii wa Wasafi wote walitemwa nje ya orodha hiyo.

Msemaji wa shirikisho la sanaa Tanzania, Steven Nyerere
Msemaji wa shirikisho la sanaa Tanzania, Steven Nyerere
Image: INSTAGRAM

Baada ya maswali mengi kuliko majibu kuibuka mitandaoni kuhusu kukosekana kwa majina ya wasanii kutoka rekodi lebo ya Wasafi katika orodha iliyotolewa na baraza la Sanaa Tanzania, BASATA, hatimaye msemaji wa shirikisho la muziki Steven Nyerere amelitupia jicho suala hilo.

Akionekana pia kulalama kuhusu kukosekana kwa wasanii wenye ushwahiba na Wasafi, Nyerere amesema kwamba kukosekana kwao katika orodha hiyo na katika vitengo tofauti tofauti kutafanya watu wengi kukosa Imani na muziki wa Tanzania.

Pia alisema suala hilo huenda litaonekana kuingizwa siasa ambapo wengi wanajua wasanii kutoka Wasafi wana rekodi za kutoa miziki mizuri tu na kukosekana ni kuwanyima haki, si wao tu bali hata wafuasi na mashabiki wao.

Ndugu zangu Viongozi wangu wa BASATA nia ya Tuzo ni Kuheshimu kazi nzuri walizo fanya Wasanii wetu kwa kipindi chote,... lakini kikubwa Zaidi Tuzo hutuunganisha watu wetu wote kuwa kitu kimoja.” Aliandika Nyerere kupitia Instagram yake.

Pia msemaji huyo amewataka BASATA kutafuta njia sahihi ya kukaa chini ya kutatua tofauti zao na uongozi wa Wasafi kwa sababu tu ya maslahi ya wasanii na Sanaa kwa ujumla, bila kushirikisha chuki na tofauti na baadhi ya watu.

“Ndugu zangu BASATA kuna haja mkaa chini tena mkajitafakari kwa hili Maana naimani vinaongeleka kwa maslahi ya Mziki wetu na mashabiki wa Mziki Tanzania. Naimani Sana na Mh Mchengelwa kwa hili naimani naye kubwa atatumia Busara kukaa kitako na @wasafi pamoja na uongozi mzima kwa Faida ya mashabiki wa mziki wetu. Kama kweli Tuna nia ya kuboresha sanaa yetu basi hakuna haja ya kuvutana kuna haja ya kukaa chini na kukubaliana na WASANIII wote kuwa tunaenda kujenga nyumba 1 haina haja ya kugombea Fito,” aliandika Nyerere.

Licha ya msanii Diamond Platnumz kuonekana hadharani kupinga uteuzi wa Nyerere katika shirikisho la Sanaa, lakini bado Nyerere ameliweka hilo kando na kupinga kuachwa nje kwa wasanii kutoka Wasafi katika orodha ya BASATA kuelekea tuzo za Tanzania Music Awards.