Zuchu: Tasnia yetu ya muziki imejaa mzaha na vichekesho

Muhtasari

• Ni Tanzania pekee ndiyo tuna industry ya muziki iliyojaa mzaha na vichekesho ndani yake - Zuchu azungumza baada ya kukosa kwenye orodha ya wawaniaji tuzo za TMA.

ZUCHU
ZUCHU
Image: INSTAGRAM

Baada ya BASATA kuwatema nje ya kuwania tuzo wasanii wote kutoka lebo ya Wasafi, hatimaye Zuchu amelizungumzia suala hilo na hisia zake kufungiwa nje ya kuwania Tanzania Music Awards.

Zuchu amelalamika kwamba tasnia ya muziki nchini humo inatia huruma sana kwani watu wengi wanaitumia kimchezo tu huku wasanii wakikosa hata kumbi maalumu za kufanya maonesho ya tamasha ya Sanaa.

“But as for the industry yetu kwa jumla inatia huruma na hasira, imagine hata sehemu ya kufanyia shoo za maana hatuna, haki zetu ndizo hizo zinachezewa sandakalawe. Tumefanywa daraja la watu wasiojali tasnia kupata umaarufu tu wa kupata kipato,” aliteta Zuchu.

Msanii huyo aliwataka wafuasi na mashabiki wa kazi zake na za wasanii wenza kutoka Wasafi kuendelea kuwapiga sapoti na pia aliwashukuru kwa umbali huu ambao wamembeba katika kuzikubali kazi zake za muziki.

Alisema wale waliohusika kutoa orodha ya wasanii wa kuwania tuzo na kuyatupa jalalani majina ya mastaa kutoka Wasafi walikuwa wanajua walichokusudia na kusikitika kwamba siasa na ugomvi usio na mashiko vimeingizwa katika mambo muhimu kama hayo.

Ni Tanzania pekee ndiyo tuna industry ya muziki iliyojaa mzaha na vichekesho ndani yake, inatia aibu maana hii mitandao tunaitumia kujichoresha kwa michezo ya kitoto tunayocheza. Mimi nawashukuru Watanzania walio wengi bila hata kushurutishwa mnajua mbivu na mbichi, mnatupambania sana wasanii wenu, that’s the only thing kinanipa nguvu kwa sababu ninyi ndiyo mnatuweka tulipo,” alisema Zuchu.