Nandy 'alia' mtandaoni baada ya kuachana na Billnass

Muhtasari

• Nandy alisema kwamba yeye hupenda kupitiliza, hivo kuwa vigumu kwake kuzuia maumivu.

• Alisema ataachana na mapenzi na kujishugulisha katika mishe zingine.

Billnass na Nandy
Image: Nandy (Facebook)

Mwanamuziki kutoka Tanzania, Nandy amedokeza kwamba ametengana na mpenzi wake, Billnass.

Kupitia ujumbe aliochapisha katika ukurasa wake wa Instagram, Nandy alisema kwamba yeye anapenda sana na hivyo kuwa vigumu kwake kuzuia maumivu.

Kwa kile kilichoonekana kama njia moja ya kumzungumzia Billnass, Nandy alisema kwamba alijitoa kwa hali na mali kuhakikisha penzi lao linasimama ila mambo yakaenda ndivyo sivyo.

Aidha alishikilia kwamba hataki tena kubembelezana katika mapenzi na kwamba anakwenda kujihusisha katika mambo mengine.

Aliongezea kwamba mapenzi ni fumbo na kama mchezo ambao mmoja lazima ashinde.

Baadhi ya wasanii mbalimbali pia walichangia huku wakionekana kukasirishwa na hali hiyo kwa kile walikitaja kwamba tayari walikuwa wamenunua nguo za kuhudhuria harusi yao.

"Nandy Nandy... Usituvuruge tunajiandaa na shughuli yenu... Please.... Acha tumalize kwanza la Tivu akee... By the time linaisha na imani wewe na mwenzako mtakuwa mshayamaliza," aliandika Wema Sepetu.

"Mpaka na sare za mahari tukashona🤦🏼‍♀️," Ammygal aliandika.

Ifahamike kwamba ni wiki chache tu zimepita tangu Billnass amchumbie Nandy, ila inaonekana kwamba kitumbua chao kimeingia mchanga kwa mara nyingine tena. 

Vilevile kuna baadhi ya mashabiki na washikadau wa buruani ambao wanaamini kwamba hiyo ni kiki ya kutengeneza mazingira mazuri ya kuachia ngoma.

Kwa sasa mashabiki watalazimika kusubiri kwa muda zaidi ili kupata taarifa kamili kutoka kwao wawili kuhusu hali hiyo.