"Ni upuzi!" Bien awakemea wanaokejeli Kiingereza duni cha Diamond Platnumz

Muhtasari

•Mbabe huyo wa muziki mwenye umri wa miaka 34 amesema kwamba umahiri wa lugha ya Kiingereza sio kipimo cha akili.

•Mwanamuziki huyo ameweka wazi kwamba atakapokuwa mzazi ni sharti atafunza watoto wake Kiluhya.

Bien na Diamond Platnumz
Bien na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki wa bendi ya Sauti Sol, Bien Aime Baraza amewakosoa wanamitandao wanaomkejeli Diamond Platnumz kwa kutokuwa na umahiri wa lugha ya Kiingereza. 

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Bien alisema kucheka Kingereza kibovu cha Diamond ni jambo la kipuzi na haifai.

"Hiyo ni upuzi! Huwa naona Wafaransa wanang'ang'ana kuzungumza Kizungu lakini huwa hamuwachekelei, Wajerumani vilevile huzungumza Kiiingereza kwa lafudhi. Watu wengi huzungumza Kiingereza kwa lafudhi, yamaanisha unajua lugha nyingine," Bien alisema.

Mbabe huyo wa muziki mwenye umri wa miaka 34 amesema kwamba umahiri wa lugha ya Kiingereza sio kipimo cha akili.

Alimpongeza sana Diamond kwa mafanikio makubwa ambayo ameweza kufanya katika taaluma yake ya usanii.

"Diamond ako na pesa. Anapiga kazi kabisa. Hao watu wanaandika vitu vya chuki nawaonea huruma tu," Alisema.

Bien alisema kwamba kujua lugha ya mama ni jambo muhimu sana. Aliweka wazi kwamba atakapokuwa mzazi ni sharti atafunza watoto wake Kiluhya.