'Madaktari walitabiri ningekufa na miaka 15,' Akuku Danger azungumzia ugonjwa ambao amekua akipambana nao

Muhtasari

•Mcheshaji huyo wa Churchill Show  alisema alikuja kufahamu kuhusu ugonjwa wake akiwa katika darasa la tano.

•Akuku amesema huwa anakumbwa na uchungu mwingi kila mara ugonjwa huo unaposhambulia tena. 

Image: INSTAGRAM// AKUKU DANGER

Mchekeshaji wa Churchill Show, Mannerson Oduor almaarufu Akuku Danger amefichua kuwa alizaliwa na ugonjwa wa Anemia ya Seli Mundu (Sickle-Cell anemia).

Akiwa kwenye mahojiano ya hivi majuzi na Mpasho, Akuku alieleza kwamba amekuwa akipambana na ugonjwa huo kwa miaka mingi

Mzaliwa huyo wa eneo la Nyanza  alisema alikuja kufahamu kuhusu ugonjwa wake akiwa katika darasa la tano.

"Nilipokuwa nakua nilikuwa naenda hospitalini mara kwa mara ili kuangaliwa. Kila mwezi lazima ningeenda hospitali. Haikuwa rahisi kwa sababu madawa yetu ni ghali," Akuku alisimulia.

Mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 31 amefichua kwamba madaktari waliwahi kubashiri kuwa angeaga akiwa na miaka 15.

"Nilipokuwa na umri wa miaka 15, daktari aliniambia na mamangu tuende nyumbani nisubiri kufa. Akamwambia wamefanya kila wawezalo. Mama yangu alikuwa mtu wa dini hivyo aliendelea kuomba. Nilimwambia mama anipeleke nyumbani na nikaomba tumpigie simu mchungaji aje aniombee, nilikuwa na maumivu makali sana lakini sikuwa amini kuwa nitakufa," Akuku alisema.

Alifichua kwamba alikua na unyanyapa mwingi hasa alipokuwa katika shule ya msingi kwani hakuchukuliwa kama watoto wengine wa kawaida.

Akuku amesema huwa anakumbwa na uchungu mwingi kila mara ugonjwa huo unaposhambulia tena.  Mojawapo ya dalili ambazo humkumba ni kubadilika kwa rangi ya macho.

Hata hivyo ameweka wazi kwamba ugonjwa huo haumshtui tena kwani tayari amezoea kuishi nao.