Mwijaku akerwa na TMA kumzawidi Diamond licha ya kujitoa kwenye tuzo

Muhtasari

• Mtangazaji mtata, Mwijaku alihoji kitendo cha shirikisho la TMA kumpa zawadi msanii Diamond Platnumz licha ya msanii huyo kujiondoa kwenye tuzo hizo zilizofanyika wikendi iliyopita.

Mwijaku, Diamond Platnumz
Mwijaku, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Mtangazaji mwenye utata Mwijaku amedhihirisha kutoridhika kwake na hatua ya msanii Diamond Platnumz kupokezwa zawadi na Tanzania Music Awards licha ya kukataa kushiriki katika tuzo hizo ambazo zilifanyika wikendi iliyopita.

Shirikisho la Sanaa Tanzania liimtambua na kumzawidi msanii Diamond Platnumz kwa mchango wake mkubwa wa kuipeleka na kuitangaza Sanaa ya muziki wa Tanzania katika nchi za kimataifa.

Ikumbukwe awali msanii huyo alijiondoa katika kupigania tuzo yoyote ya TMA, hafla ambayo ilimpa mbaya wake wa siku zote, Alikiba nafasi kubwa ya kutamba kwa kujinyakulia tuzo tano katika vitengo tofauti.

Mtangazaji ambaye pia anajiita kama DC wa Instagram, Mwijaku hakufurahia kwa urahisi hatua ya shirikisho la TMA kumtambua Diamond ambapo aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter na kulalama kwamba haiwezekani mnazidi kumtambua mtu ambaye hatambui kazi na michongo yenu.

“Kuna kitu  kwenye tuzo za #TMA sijapenda. Mnatoaje tuzo kwa mtu ambaye hakubali mchakato wenu? Mmenikwazaaa,” aliteta Mwijaku.

Mtangazaji huyo ana mazoea ya kumkosoa msanii Diamond katika kila jambo ambalo analifanya ila anadai msanii Diamond ndiye Rafiki yake mkubwa licha ya kumkosoa kwa sana.

Mapema mwaka huu wakati Wasafi Bet ilipokuwa ikizinduliwa, wengi walishangaa kumuona Diamond akimpabidhi ubalozi Mwijaku licha ya Mtangazaji huyo kuwa na msururu wa kumtupia maneno.