Size 8 afunguka kuhusu ugonjwa ambao amekuwa akipambana nao kufikia hatua ya kufa moyo

Muhtasari

•Ugonjwa huo ulitambulika baada yake kuzirai mtaani alipokuwa anaelekea nyumbani baada ya kutumbuiza katika tamasha.

•Alikiri kwamba hivi majuzi ugonjwa huo ulikuwa umemwathiri kiasi cha kupatwa na msongo wa mawazo na kutaka kukata matumaini ya maisha.

Mwimbaji wa nyimbo za injili Size 8
Mwimbaji wa nyimbo za injili Size 8
Image: INSTAGRAM// DJ MOH

Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili, Linet Munyali almaarufu Size 8 amefichua kwamba amekuwa akipambana na shinikizo la damu zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Size 8 ambaye alitawazwa kuwa mhubiri mwishoni mwa mwaka jana amesema aligunduliwa kuwa na ugonjwa huo mnamo Januari 31, mwaka wa 2015.

Ugonjwa huo ulitambulika baada yake kuzirai mtaani alipokuwa anaelekea nyumbani baada ya kutumbuiza katika tamasha ambayo alikuwa amehudhuria pamoja na mumewe, DJ Moh.

"Nilizirai nikiwa mjini nikapelekwa katika hospitali moja iliyokuwa pale. Hapo ndipo nikaambiwa shinikizo la damu yangu ni kubwa mno. Nilikuwa siko sawa. Kutoka siku hiyo nilianza kuchukua dawa za shinikizo la damu," Size 8 alisimulia kupitia YouTube channel ya 'The Murayas'

Mama huyo wa watoto wawili alisema ugonjwa huo umekuwa ukimzidia mara kwa mara na kumfanya alazwe hospitali mara kadhaa tangu ulipogunduliwa.

Alisema amekuwa akipambana nao kwa ujasiri. Hata hivyo alikiri kwamba hivi majuzi ugonjwa huo ulikuwa umemwathiri kiasi cha kupatwa na msongo wa mawazo na kutaka kukata matumaini ya maisha.

"Mara hii haikuwa rahisi kwangu. Nilihisi nilikuwa nazama kwenye msongi wa mawazo.Kama sio neema ya Mungu nadhani ningekufa moyo kabisa.. Nilihisi kama kwamba nimechoka kupambana, nimechoka kuendelea, nimechoka kusubiri, nimechoka kusubiri muujiza. Mara nyingi sikuwa nahisi vizuri. Kuna wakati Moh alikuja katika chumba cha malazi na nikamwambia sihisi poa na nahisi kukata tamaa. Hiyo ni baada ya kutoka hospitali. Tulishiriki naye mazungumzo marefu," Alisema.

Size 8 alisema DJ Moh amekuwa guzo muhimu katika mapambano yake na shinikizo la damu. Alisema mumewe amekuwa akimtia moyo na kumsihi asikate tamaa.

Mwaka jana, mwanamuziki huyo alipoteza ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wao wa tatu kutokana na shinikizo la damu.

Wiki chache zilizopitwa, Size 8 alikimbizwa katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kukumbwa na ugonjwa huo.