Harmonize ashauriwa kuzingatia haya ili kumshinda Diamond katika muziki na utajiri

Muhtasari

• Muda hufika ambapo msanii wako pendwa huondoka stejini na kuacha kuimba muziki, na lazima pengo lake lizibwe hata kama ni kwa kubambanya.

• Baada ya kutathmini kwa muda, wengi wanampigia upato msanii Harmonize kuliziba pengo litakaloachwa na Diamond wakati atashuka viwango vya muziki mzuri.

Diamond na Harmonize
Diamond na Harmonize
Image: Screengrabs: YouTube

Kama ilivyo kawaida, kwenye maisha, kila mtu ana nafasi au zamu yake ya kung’ara na kutaradadi. Ndivyo ilivyo katika maisha ya kila mtu haijalishi taaluma ama kitivo.

Katika ukanda wa Afrika mashariki, tasnia ya Sanaa ndio inaendelea kukua kila uchao, huku wasanii wapya wakikaribishwa katika taaluma hiyo kila siku huku mamia ya wengine wakitoka na kubadilisha taaluma baada ya Sanaa kuwa mbinde.

Itakumbukwa tangu enzi za mwaka 2000, pamekuwepo na wasanii mbalimbali tena wazuri wenye talanta na sauti nzuri za kuimba na kutunga mashairi ajabu. Lakini wote hao kama ilivyo kawaida huhanikiza kwa muda wao kama vile maua na kisha kunyauka.

Tukizamia tasnia ya muziki Tanzania kwa mfano, paliwahi tokea wasanii wazuri tu kama vile Mr Nice, Juma Nature, akaja AY miongoni mwa wengine. Ni uongo kusema hawakufana na kuvuka mipaka mpaka kuijenga heshima ya majina yao katika mawimbi ya mataifa Jirani.

Lakini pia muda wao wa kuondoka kwenye steji ulipofika walisepa na kuwapisha wasanii wapya kina Alikiba, Diamond na wengine wengi ambao wameendeleza mbingiriko wa gurudumu hilo mpaka hivi sasa.

Hawa pia ni binadamu na muda wao bila shaka utafika, sasa mijadala mitandaoni ni kuhusu wale watakaovalia viatu vya wasanii wakubwa kwa mfano Diamond pindi mchezo wake wa usanii utakapomuonesha kodi nyekundu.

Baada ya kutathmini kwa muda, wengi wanampigia upato msanii Harmonize kuliziba pengo litakaloachwa na Diamond wakati atashuka viwango vya muziki mzuri.

Lakini pia licha na Harmonize kupigiwa upato, bado ana kazi kubwa sana ya kuifanya na kulingana na mdau mmoja kutoka taifa hilo anayekwenda kwa jina Hope Tyga kwenye Instagram, Harmonize ana mambo mengi tu anayostahili kuyazingatia ili kurithi nafasi ya Diamond kimziki.

Tyga anaamini ipo siku moja tu ambapo Harmonize atampindua Diamond na umaarufu pamoja na utajiri wake utazidi hata ule wa sasa wa Diamond, ila ameorodhesha mambo yafuatayo Matano yanayomhusu Harmonize kama anapania kupiku rekodi za Diamond.

  1. ASITEGEMEE HURUMA YA WATANZANIA. Harmonize aache kuanika mabaya ya Diamond ili tu Watanzania wamuonee Huruma, afunge domo lake asimuongelee vibaya Diamond, Hii itamsaidia kupata mashabiki wengi zaidi.
  2. AKUBALI KWAMBA DIAMOND ANAMCHANGO MKUBWA KATIKA MUZIKI WAKE. Yes, Juzi nimeona Harmonize kaacha unafiki na akakubali kabisa kwamba bila Diamond yeye asingekuwa hapo. Hii ni nzuri sana na inabidi asisahau kabisa umuhimu wa Diamond, hii pia itamsaidia kupata mashabiki na baraka tele.
  3.  APUNGUZE KIKI ZA KISHAMBA. Harmo asiendekeze kiki za kijinga, zinampotezea sana mashabiki, pia watu wengi wataanza kumpuuza na wamuone kama mtoto vile, afanye kazi, asiendekeze kiki
  4. AKOMAE KIAKIRI. Kuna collabo Harmonize anafanya hazina faida, mfano ile ya mabantu, Hii omoyo pia, yani anakurupuka mno, inabidi aangalia kimataifa zaidi, afocus mbele, asiendelee kunga'nga'na hapa hapa Tanzania, Diamond aliamua kabisa kuvuka boda na akafanikiwa kweli, so Harmonize afuate nyayo hizo.
  5.  HARMONIZE ASIWE KAMA ALIKIBA. Yani katika vitu muhimu kabisa, isije ikatokea Harmonize akawa na bifu zito na Diamond kama ambavyo Alikiba na Diamond walivyo, yani ikibidi Harmonize amalize bifu kabisa na Diamond, maana Diamond anamashabiki wengi, ukijenga nae bifu, watu kibao watakukataa na hautaendelea kimuziki, so Harmonize Afanye juu chini bifu lake na Diamond lisiwe kubwa sana.

 

Sijui wewe ungependa kumuongezea Harmonize ushauri upi kando na haya Matano kutoka kwa mdau, au unakubaliana na mangapi kati ya haya aliyoshauriwa Harmonize kufanya.