Mabinti wa Akothee wamsherehekea kwa jumbe maalum huku akitimiza miaka 41

Muhtasari

•Akothee amejitambua kama mtu mchangamfu, mbunifu, mwajibikaji, mjasiri, mwaminifu, mnyenyekevu, mwenye maarifa na mwenye kupenda.

•Fancy Makadia ambaye ni mtoto wa tatu wa msanii huyo amesema siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa mama ndiyo muhimu sana kwenye kalenda yake.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee alizaliwa siku kama ya leo (April 10) takriban miongo minne iliyopita.

Mwaka huu, mama huyo wa watoto watano anaadhimisha miaka 41 tangu alipozaliwa katika eneo la Nyanza.

Akothee amejitambua kama mtu mchangamfu, mbunifu, mwajibikaji, mjasiri, mwaminifu, mnyenyekevu, mwenye maarifa na mwenye kupenda.

"Kheri za kuzaliwa minwa, upendo nilio nao kwako si wa hapa duniani. Barikiwa sana min oyoo. Nakupenda," Akothee amejiandikia kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Binti wa kwanza wa mwanamuziki huyo, Vesha Okello amebainisha kwamba mzazi huyo wake  ametekeleza jukumu lake la mama ifaavyo.

"Yeye ni mjasiri, mbunifu, mwenye upendo, anayefanya kazi kwa bidii. Lakini zawadi yake kubwa ni kuwa mama.  Kheri za siku ya kuzaliwa kipenzi changu. Wewe ni nyota inayong'aa. Hadi ukiwa na miaka 41  bado wewe ni mzuri. Unazeeka kama mvinyo mzuri," Vesha alimwandikia mamake.

Rue Baby kwa upande wake amemtaja mamake kama mtu jasiri zaidi aliwahi kukutana naye maishani.

"Mwaka huu mpya kwako naomba upate upendo na baraka. Kheri za kuzaliwa mama. Nakupenda mama," Aliandika.

Fancy Makadia ambaye ni mtoto wa tatu wa msanii huyo amesema siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa mama ndiyo muhimu sana kwenye kalenda yake.

"Kuna siku 365 kwa mwaka lakini siku yako ya kuzaliwa inang'aa zaidi kuliko zote. Kheri za siku ya kuzaliwa mama," Alisema.

Mamia ya mashabiki wa Akothee wameendelea kumwandikia jumbe za kheri njema za siku ya kuzaliwa.