Karen Nyamu bado anampenda Samidoh, aonekana na ushanga wake mkononi

Muhtasari

• Mwanasiasa Karen Nyamu wikendi iliyopita alionekana na ushanga mkononi uliokuwa na jina la aliyekuwa mpenzi wake Samidoh.

• Hilo lilizua mjadala mkali mtandaoni baadhi wakihisi bado anampenda baba wa watoto wake wawili, Samidoh.

Karen Nyamu
Karen Nyamu
Image: Facebook

Mwanasiasa Karen Nyamu ambaye alikuwa analenga kuwania Useneta wa Nairobi kupitia tiketi ya chama cha naibu rais William Ruto, UDA wikendi iliyopita amezua gumzo mitandaoni baada ya kuonekana na bangili ya ushanga mkononi mwake ikiwa na jina la msanii Samidoh.

Kwenye msururu wa picha ambazo Nyamu alipakia kwenye Ukurasa wake wa Facebook katika hafla moja ya kampeni, mwanasiasa huyo anaonekana na ushanga huo wenye jina kubwa tu la msanii wa Mugithi, Samidoh ambaye ni baba wa watoto wake wawili aliozaa naye nje ya ndoa.

Ikumbukwe miezi michache iliyopita kabla ya kujifungua mtoto wake wa pili, Nyamu na Samidoh walizushiana mitandaoni ambapo walipapurana kwa jumba fiche huku Samidoh akidai mtoto huyo aliyetarajiwa si wake naye Nyamu akijibu kwamba hajamshrutisha kutekeleza malezi kwa mtoto huyo.

Tukio la Nyamu kuwa na mimba ya pili ya msanii Samidoh lilisababisha ndoa ya msanii huyo kuvunjika ambapo pia Nyamu naye alimbwaga na kuleta tafsiri ya msemo kwamba mpanda farasi wawili hakika hupasuka msamba na mdakia mawili sharti moja limponyoke.

Baada ya wengi kuamini kwamba wawili hao waliachana kwa kutupiana maneno, Nyamu alichanganya mashemeji wa mitandaoni kwa kuonekana na ushanga huo ambao kwa kiasi kikubwa ulionesha kwamba huenda bado anampenda sana Samidoh kwani haiwezekani uvalie kitu chenye jina la mbaya wako.