Akothee ajivunia mabinti zake kwa kupata digrii bila kupachikwa mimba

Muhtasari

•Akothee amejipongeza kwa kufanikiwa kuwalea mabinti zake watatu hadi kufikia kupata degree bila wao kuwahi beba ujauzito.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Kipindi cha siku kadhaa ambacho kimepita, mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amekuwa akifurahia wakati pamoja na familia yake.

Watoto watatu wa mwisho wa malkia huyo wa burudani walitua nchini Jumamosi kutoka Ufaransa ambako wamekuwa wakiishi.

Akothee ambaye aliandamana na mpenziwe Nelly Oaks na binti zake Vesha Okello na Rue Baby kuwapokea watatu hao aliwezwa na hisia alipowaona kwa mara ya kwanza baada ya miezi minane.  

"Imekuwa miezi 8. Ni muda mrefu sana kusubiri wakati huu. Mungu awatie nguvu wazazi wote wanaofanya kazi mbali na familia zao ili kujikimu kimaisha," Akothee alisema kupitia Instagram siku ya Jumamosi.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 41 amekuwa akipakia picha zinazoonyesha akijivinjari na watoto wake.

Katika chapisho lake moja, Akothee amejipongeza kwa kufanikiwa kuwalea mabinti zake watatu hadi kufikia kupata degree bila wao kuwahi beba ujauzito.

"Kujeni muone fahari yangu Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia. Wote wamepata degree bila ujauzito. Alafu mseme mimi sio mfano wenu kwenye jukumu hili. Lakini si myoto ni mtoto tu," Akothee aliandika chini ya picha yake na mabinti zake.

Fancy Makadia ndiye binti wa mwisho wa Akothee kumaliza masomo ya chuo kikuu. Alikuwa anasomea katika chuo kimoja cha kifahari jijini Paris, Ufaransa.

Rue Baby alipata shahada yake Disemba mwaka jana, takriban mwaka mmoja baada ya dadake mkubwa Vesha Okello kuhitimu.