Mchekeshaji YY achangisha zaidi ya 100K chini ya saa 4 kumsaidia jamaa aliyeiba vyakula Naivas

Muhtasari

• YY: Ahsante sana Wakenya, tumefikia malengo yetu na hata tumezidi, kijana tutamtoa na pesa zote atapewa anunue mafuta vile anataka ili asiibe

YY Comedian, Alvin Linus Chivondo
YY Comedian, Alvin Linus Chivondo
Image: Facebook, Maktaba

Mchekeshaji YY aliwaongoza wakenya Jumatano kuchangisha pesa mitandaoni ili kufidia faini aliyotozwa kijana mmoja aliyepatikana akiiba vyakula katika duka la jumla la Naivas jijini Nairobi.

YY aliguswa na suala kwamba jamaa huyo kwa jina Alvin Chivondo mwenye umri wa miaka 21 alitekeleza kitendo hicho kutokana na makali ya njaa yaliyoishambulia familia yake na kusema kwamba mtoto wake wa miezi minne alikuwa amekaa siku kadhaa bila kutia kitu kinywani ndiposa akafanya kufuru hiyo ya kuiba.

“GUYS NIMEONGEA NA MTU ALIYE MILIMANI ANAYEJUA LInus yuko karibu na eneo la viwanda!!!! Kwa kuwa hatujapata ripoti zozote kutoka kwa familia, tuone kama tunaweza kufikia 100k kufikia kesho tunaenda na Tumtoe….na tumnunulie chochote anachohitaji. 0768062102…Jina ni Oliver...Nitasasisha kila sarafu…na pia nitahamasisha marafiki zangu….Twende!!!!!!” YY aliwasihi Wakenya mitandaoni.

Mahakama ya Milimani ilimtoza faini ya laki moja pesa za Kenya au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa hilo. Hili liligusa wakenya wengi ambao walijitolea kusimama naye kwa kumchangia pesa hizo kama faini ili awe huru na pengine kumtafutia maisha ili aweze kumlea mwanawe.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko baadae alitoa ahadi ya kumlipia kijana huyo faini hiyo yote na pia akaahidi kumnunulia chakula cha kuisukuma kwa miezi kadhaa na kumtafutia kazi ya kujikimu kimaisha.

Hatua hii nzuri kutoka kwa Sonko hata hivyo haikusitisha kile kilichoanzishwa na mchekeshaji YY kwani watu walizidi kutuma michango yao ambapo chini ya saa kumi tu Wakenya walikuwa wamechangisha zaidi ya laki moja.

YY alisema kwamba japo Sonko amegharamia faini hiyo, pia wao watampokeza Chivondo pesa hizo ili kujiendeleza zaidi kimaisha.

Alvin Chivondo alishtakiwa katika mahakama ya Milimani Jumatano kwa kosa la kuiba lita tano za mafuta ya kupika, sukari, mchele na majani chai vyote vilivyogharimu shilingi 3,165 za Kenya.