Kama hawakusaidii hao sio rafiki zako, Jalang'o afunguka ya moyoni

Muhtasari

• Jalang'o amesema kwamba iwapo watu wako wa karibu hawakusaidii katika kipindi cha uhitaji, basi hao sio rafiki.

• Alikuwa akiyazungumza hayo katika mahojiano na wanablogu baada ya kufungua rasmi mkahawa wa mkewe jijini Nairobi.

Jalango
Jalango
Image: Hisani

Mwanasiasa Felix Odiwour almaarufu Jalang'o amesema kwamba iwapo wandani wako hawakusaidii wakati wa uhitaji, basi hawapaswi kuwa rafiki zako.

Akizungumza na wanablogu katika mkahawa mpya wa mkewe [Wapekdelcacies], Jalang'o alisema kwamba rafiki wa kweli atashawishika kutoa msaada bila kulazimishwa.

"...Kama hawezi kusaidia basi huyo sio rafiki tena, sema ni mtu tu wa kawaida ambaye mnafahamiana naye. Labda wewe tu ndo umekuwa ukifikiria kwamba wao ni rafiki zako" Jalang'o alisema.

Aliwataja rafiki zake kama vile gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, kinara wa ODM Raila Odinga, Oga Obinna, Kamene Goro miongoni mwa wengine ambao lazima watatoa sapoti katika safari hiyo ambayo ameianza na mkewe.

Alisema kwamba kuna baadhi ya rafiki ambao watataka kukupaka tope wakati unapopitia changamoto ila lazima kama mtu binafsi ujue jinsi ya kutofautisha rafiki wa kweli na wale wanafiki.

Aidha, alisema kwamba wale ambao wanasema ni maadui wake, anawatafsiri kama mashabiki wake ambao wamechanganyikiwa.

Jalang'o alidokeza kwamba mkahawa huo utakuwa unajikita katika vyakula vya kiasili kando na mikahaa mingine iliyoko katikkati mwa jiji.

Odiwour atakuwa anawania ubunge wa Lang'ata kupitia tikiti ya chama cha ODM, huku kura za mchujo chamani humo zikitarajiwa kufanyika Alhamisi.

Anaamini kwamba atashinda kura hizo kwa kuwa tayari ameshauza sera zake kwa wakazi na wanaonekana kumuunga mkono.