"Kifo chake kiliniua sana!" Njoro afunguka kuhusu majonzi ya kufiwa na Papa Shirandula

Muhtasari

•Njoro amekiri aliwezwa sana na hisia kufuatia kifo cha mwigizaji huyo mwenzake mnamo Julai 18, 2020.

•Njoro amefichua kwamba hakupata nafasi ya kumwona marehemu kwa mara ya mwisho ili kuwa na 'kifungo'

Njoro na Papa Shirandula
Njoro na Papa Shirandula
Image: HISANI

Mwigizaji Kenneth Gichoya almaarufu Njoro kutokana na kipindi cha Papa Shirandula amefichua kwamba kifo cha aliyekuwa bosi wake Charles Bukeko kilimvunja moyo sana.

Njoro amekiri aliwezwa sana na hisia kufuatia kifo cha mwigizaji huyo mwenzake mnamo Julai 18, 2020.

"Alikuwa mtu mmoja kati ya milioni. Kifo chake kiliniua sana. Sio watu wetu wengi ambao nimewahi kulia juu yao, lakini huyo nililia sana juu yake. Sikujua machozi yalikuwa yanatoka wapi lakini nililia sana," Njoro alisema katika mahojiano na Ala C.

Mwigizaji huyo alisema alilia kwa kuwa hakuwa anaamini kwamba safari ya Papa Shirandula duniani ilikuwa imefika kikomo.

Njoro alifichua kwamba hakupata nafasi ya kumwona marehemu kwa mara ya mwisho ili kuwa na 'kifungo'

"Nilikuwa katika hali ya kukataa. Sikuwa naamini. Ungeona machozi yakitiririka kwa kuwa sikuwa nimeanza kuomboleza," Alisema.

Katika kipindi cha Papa Shirandula, Njoro aliigiza kama rafiki wa karibu zaidi wa marehemu Charles Bukeko.

Njoro amesema ataishi kumkumbuka marehemu kutokana jinsi alivyokuwa na imani kubwa kwake na alivyomsaidia katika masuala mbalimbali.

"Kazini nilikuwa nakosea mara kwa mara. Alikuwa anasimama nami. Hata kampuni ikisema inataka kunifuta, alikuwa anasema siendi mahali. Hata katika masuala ya familia, alikuwa ananisaidia tukikosana na watu wangu angekuja na kunisaidia kupatana nao," Alisema.

Njoro vilevile aliwakosoa watu waliomkejeli kutokana na mahangaiko yaliyomkumba kutokana na kifo cha Bukeko.