Aika wa Navy Kenzo afanyiwa upasuaji wa goita ambayo amekuwa akiishi nayo miaka mingi

Muhtasari

•Aika amesema kwamba shughuli ya upasuaji iliendelea vizuri na kwa sasa anaendelea kupata afueni.

•Aika alisema aligunduliwa kuwa mwathiriwa wa goita baada ya mamake  kumsihi aende akapimwe.

Image: INSTAGRAM/ AIKANAVY KENZO

Mwanamuziki Aika Marealle wa bendi maarufu Bongo, Navy Kenzo amefanyiwa upasuaji wa kurekebisha tatizo la goita ambalo amekuwa akiishi nalo.

Hivi majuzi malkia huyo wa muziki alifichua amekuwa akiishi na tatizo hilo kwa miaka mingi ila hakuwa na ufahamu.

Aika amesema kwamba shughuli ya upasuaji iliendelea vizuri na kwa sasa anaendelea kupata afueni.

"Shukran kwa jumbe zenu, nimetoka upasuaji salama Naomba niweze kupona vizuri. Namshukuru Mungu na madaktari," Aika alitangaza Jumapili kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Akihutubia mashabiki wake hivi majuzi, Aika alisema aligunduliwa kuwa mwathiriwa wa goita baada ya mamake  kumsihi aende akapimwe.

"Nilidhani mimi ni mnene. Siku moja nikapiga picha na dadangu na watu wakasema shingo zetu nzuri kweli mashallah. Mashabiki wakawa wananiambia kwa DM kuwa nitakuwa na goita. Tulipokutana na mamangu wakati mmoja aliniambia niko na goita niende nikapimwe na nikaenda," Aika alisema.

Mwanamuziki huyo alisema alikuwa anasubiri kukamilika kwa albamu yake ili aweze kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha hali hiyo.

Hali kadhalika Aika amewahimiza mashabiki wake kuweza kupimwa hali ya goita huku akisema kuwa wengi wanaishi nayo bila kujua.