Muigizaji wa Vioja Mahakamani ahitaji msaada wa kifedha ili kupandikizwa figo

Muhtasari

•Muigizaji Gibson Gathu 'Prosecutor' amekuwa akipambana na ugonjwa wa sukari kwa zaidi ya miongo miwili.

•Familia imesema kuwa fedha wanazoziomba zinajumuisha gharama za upasuaji na matibabu ya baadae.

Mwigizahi wa Vioja Mahakamani Gibson Gathu
Mwigizahi wa Vioja Mahakamani Gibson Gathu
Image: HISANI

Muigizaji Gibson Gathu mashuhuri kutokana na kipindi cha Vioja Mahakamani ametoa wito kwa wasamaria wema kumsaidia kuchangisha Ksh6 milioni kwa ajili ya matibabu ya figo.

Gathu ambaye alicheza nafasi ya kiongozi wa mashtaka katika kipindi cha Vioja Mahakamani amekuwa akipambana na ugonjwa wa sukari kwa zaidi ya miongo miwili.

Familia yake imesema matibabu yake yamewasababisha matatizo ya kifedha na hivyo wanahitaji kusaidiwa kuchanga pesa za kugharamia upasuaji utakaofanyika Julai 22, 2022.

"Gib amekuwa akipambana na ugonjwa wa sukari kwa zaidi ya miaka 20. Mwezi Novemba 2020m figo zake zilikosa kufanya kazi na amekuwa akienda kupokea matibabu ya dialysis mara mbili kwa wiki. Hii imesababisha shida za fedha katika familia," Tangazo lililofikia Radio Jambo lilisoma.

Familia ya muigizaji huyo imesema kwamba tayari amepata mtu wa kumtolea figo moja. Wamesema kuwa fedha wanazoziomba zinajumuisha gharama za upasuaji na matibabu ya baadae.

"Hafla ya kuchangisha itafanyika Juni 11, 2022 katika City Hall, Nairobi kuanzia saa nane mchana. Uwepo wako utathaminiwa sana," Tangazo hilo lilisoma.

Wakenya wameombwa kumchangia msanii huyo kupitia nambari ya Lipa na M-pesa:247247, nambari ya akaunti 777626.