Flossin Mauwano asimulia machungu ya kushuhudia wazazi wake wakifariki katika ajali ya barabarani

Muhtasari

• Flossin Mauwano alifichua kuwa wazazi wake wawili waliangamia katika ajali ya barabarani akiwa bado katika shule ya msingi.

•Alisema kuwa mamake aliaga papo hapo baada ya kuangukiwa na kupondwa na gari lao lililohusika katika ajali.

Image: INSTAGRAM// FLOSSIN MAUWANO

Mchoraji Stephen Mulee almaarufu Flossin Mauwano amefunguka kuhusu maisha yake magumu ya utotoni. 

Akiwa kwenye mahojiano na Ala C, Flossin Mauwano alifichua kuwa wazazi wake wawili waliangamia katika ajali ya barabarani akiwa bado katika shule ya msingi.

Msanii huyo alisema wazazi wake walipata ajali katika barabara ya Langata walipokuwa wanajaribu kukwepa ghasia za baada ya uchaguzi wa 1997.

"Tulikuwa na nyumba za kukodisha Kibera lakini tulikuwa tunaishi Langata. Wazazi wangu walikuwa wanatoka kwa nyumba zetu zilizo Kibera  wakikuja nyumbani Langata. Watu walianza vita. Katika ile harakati ya kutoroka gari lao likapata ajali wakaaga," Flossin alisimulia.

Baada ya kufikiwa na habari za ajali hiyo, Flossin alikimbia katika eneo la tukio bila kujali ghasia zilizokuwa zinaendelea na kujaribu kuokoa babake.

Alisema kuwa mamake aliaga papo hapo baada ya kuangukiwa na kupondwa na gari lao lililohusika katika ajali.

"Nilikuwa napenda babangu sana nikaamua kubahatisha. Nilipata babangu akiwa kwa mtaro nikamtoa nikambeba . Aliendelea kuwa baridi kama nimemshika. Akanyamaza hata hakuitika nikimuita. Baadae ndio polisi walikuja mwendo wa saa usiku. Huo muda wote nilikuwa nimemshika babangu nikisubiri usaidizi," Alisimulia.

Flossin alisema baada ya wazazi wake kuaga alilazimika kuishi na mama yake wa kambo ambaye alimtesa sana alipokuwa anakua.

Alifichua kuwa kifo cha wazazi wake katika ajali kilimshinikiza kuanzisha kampeni ya kutetea usalama wa barabarani.