Nilisahau kuimba- Mwanamuziki Nyota Ndogo afichua

Muhtasari

•Nyota Ndogo amedai kuwa mashabiki wake wengi wamekuwa wakimshawishi sana arudi studioni.

•Mwanamuziki huyo kutoka eneo la Pwani amedokeza kuwa anapanga kufanya ziara kwa vyombo vya habari.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo ameweka wazi kwamba kwa sasa hana uwezo wa kutengeneza muziki mpya.

Mama huyo wa watoto wawili amedai kuwa mashabiki wake wengi wamekuwa wakimshawishi sana arudi studioni.

Nyota Ndogo amebainisha kuwa kwa sasa anaangazia  hoteli yake huku akiwasihi mashabiki wake kupromoti biashara hiyo yake.

"Naona mashabiki wanasema nitoe nyimbo sasa mwenyewe nilisahau kuimba.njooni hotelini kwangu munipromoti chakula napika vizuri sana," Nyota Ndogo amesema kupitia Instagram.

Mwanamuziki huyo kutoka eneo la Pwani amedokeza kuwa anapanga kufanya ziara kwa vyombo vya habari.

Hata hivyo ametoa ombi kutohojiwa kwa Kiingereza huku akifichua kuwa hana uwezo wa kuzungumza lugha hiyo.

"Huwa nakiongea vizuri kimoyo moyo lakini nikifungua mdogo balaa. Lakini kadri nakiongea nikama mazoezi vile nafikiria nimefungua Radio Nyota nikiongea Kingereza. Simtakufa na vicheko, lakini mimi sijali nitakaza," Alisema.

Nyota Ndogo alijitosa kwenye tasnia ya muziki zaidi ya miongo miwili iliyopita na alikuwa maruufu sana kati ya 2000-2010.

Hataweza kutoa kibao chochote miaka ya hivi majuzi.