"Nafurahia ana mahali pa kuita nyumbani" King Kaka amjengea mamake jumba la kifahari

Muhtasari

•King Kaka amepakia nyumba maridadi aliyomjengea mamake na kufichua ilizinduliwa mapema wiki hii.

•Amesema jumba hilo ni utimilifu wa ahadi aliyompatia mamake miaka mingi iliyopita baada ya nyumba waliyokuwa wamekodisha kufungwa kwa kutolipa kodi ya Sh500. 

King Kaka na mama yake
King Kaka na mama yake
Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Huku siku ya kusherehekea kina mama duniani ikiwadia, rapa maarufu King Kaka amefichua kuwa mama yake amehamia katika nyumba mpya ambayo alimjengea.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, King Kaka amepakia nyumba maridadi aliyomjengea mamake na kufichua ilizinduliwa mapema wiki hii.

"Siku nne zilizopita, tuliomba sebuleni ya nyumba hii ambayo nilimjengea. Sauti ya ushuhuda na nafurahia kuwa ana mahali pa kuita nyumbani," Kaka ameandika chini ya picha ya nyumba hiyo ya mawe.

Jumba hilo la mawe la ghorofa moja limejengwa katika uwanja mkubwa na limezingirwa na mazingira mazuri sana.

King Kaka amesema jumba hilo ni utimilifu wa ahadi aliyompatia mamake miaka mingi iliyopita baada ya nyumba waliyokuwa wamekodisha kufungwa kwa kutolipa kodi ya Sh500. 

"Siku moja nilirudi kutoka shuleni na Kanjo alikuwa ameweka kufuli Kubwa sana juu hatukuwa na uwezo wa kulipa kodi ya Kshs 500, nilimuahidi mama yangu kuwa siku zijazo nitamnunulia nyumba," Kaka amesema.

Mwanamuziki huyo amemshukuru mama yake kwa kuonyesha ujasiri mkubwa katika hali zote za maisha.

Pia amewasihi watu kutokufa moyo katika mambo ambayo wanaamini na kuwa na imani kubwa kwa Maulana.

Jumapili ijayo, Mei 8 itakuwa siku ya kuadhimisha kina mama kote duniani.

Kwa kawaida, watu wengi hutumia fursa hiyo kuwasherehekea kina mama zao kwa njia tofauti tofauti.

Miongoni mwa mambo ambayo watu huwafanyia mama zao ni pamoja na kuwapatia zawadi kubwa, kuwaandalia karamu, kuwapeleka likizo, kuwatembelea na mengineo.

Ni vyema kuwasherehekea kina mama zetu kwa kuwa wao ndio walifanikisha kuwasili kwetu hapa duniani.