"Mumetuonea!"Diamond na Zuchu wavunja kimya baada ya video yao kupigwa marufuku

Muhtasari

•Zuchu amekiri kuwa yeye ndiye aliyeelekeza kipande cha video hiyo ambacho kimezua tashwishi.

•Zuchu ameilalamikia Basata kwa kuifungia video hiyo na kuwashtumu kwa kuangamiza tasnia ya muziki ya Bongo.

•Diamond ameikosoa Basata kwa kufungia video yao huku akidai kuwa hakuna uovu uliofanyika ndani ya kanisa.

Diamond Platnumz na Zuchu
Diamond Platnumz na Zuchu
Image: HISANI

Hatimaye mastaa wa Bongo Diamond Platnumz na Zuchu wamejitokeza kutoa majibu kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) baada ya kuipiga marufuku video ya wimbo wao 'Mtasubiri'.

Basata iliipiga hatua hiyo kufuatia malalamishi ya baadhi ya waumini kuhusu kipande cha video hiyo kinachodaiwa kuleta ukakasi kwenye jamii husika.

Kikundi cha waumini kiliwasilisha ombi la kufutwa kwa video hiyo wakidai kuwa kuna kipande ambacho kinaashiria dharau kwa dini fulani.

"Msanii tajwa (Diamond Platnumz) ametoa video ya wimbo unaofahamika kama 'Mtasubiri Sana' na katika video hiyo kuna kipande kimeonyesha wahusika wapo kanisani wanaimba kwaya lakini baadae wakaacha na kuelekea kwingine. Kipande hicho cha video kimeleta ukakasi miongoni mwa waumini wa madhebehu ya dini na kuleta hisia kwamba ni dharau ya dini/madhebehu fulani," Taarifa iliyopigwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA Dkt Jabiri K. Bakari ilisoma.

Akizungumza baada ya hayo, Zuchu amekiri kuwa yeye ndiye aliyeelekeza kipande cha video hiyo ambacho kimezua tashwishi.

Amesema kuwa watawa wa kanisa husika waliwaruhusu kurekodi video yao pale baada ya kusikiliza wazo lao na kuridhishwa nalo.

"Nafahamu si kila kazi ya kisanaa itamfurahisha kila mtu lakini kuvunjia heshima dini si kitu ambacho kipo ndani ya weledi wa kazi yetu sababu tunafahamu fika tunao mashabiki wa dini zote na kulinda hisia zao ni moja ya nguzo kuu Kwenye mziki hatueki matabaka .Ifahamike kwamba mimi ndie nilishoot hiyo scene ikinataka kuwepo kanisani nikiwa nafanya mazoezi ya kwaya sio misa ni mazoezi ya kikwaya nikiwa nimevalia joho lenye stara .Kanisa hili lipo kisarawe na kabla ya kushoot masister walitukagua na kusikiliza kwa makini stori yetu na kuridhishwa nayo ndipo hapo tukapewa ruhusa ya kushoot," Zuchu amesema kupitia Instagram.

Malkia huyo wa muziki amesema kuwa amechukua muda wake kutazama video ya wimbo huo tena ila hajaweza kuona ukakasi unaoongelewa.

Zuchu ameilalamikia Basata kwa kuifungia video hiyo na kuwashtumu kwa kuangamiza tasnia ya muziki ya Bongo.

"Huu ndio umauti wa Tasnia hii unapoanzia .Sijui nileleze vipi hisia zangu zipokelewe kwa heshima ya kutosha na utii bila ya kuchukuliwa kama mjeuri ila kwa hili mumetuonea .Sisi ni vijana tunaotafuta rizki bila ya kuchoka lakini pengine Wazazi wetu BASATA mmekua mstari wa mbele kutuvunja nguvu mbele ya jamii bila kujali hisia muda vipaji na uwekezaji unaofanyika," Amesema.

Diamond kwa upande wake ameikosoa Basata kwa kufungia video yao huku akidai kuwa hakuna uovu uliofanyika ndani ya kanisa.

"Najiuliza kuna baya lolote limefanyika kwenye hio scene? Mlivaa vimini? hapana!… Nlitwerk ama Mliimba matusi humo kanisani? Hapana!.. Mlivuta sigara au bangi humo? Hapana!… Mlikiss ama Kunywa Pombe humo Hapana!… Simu iliita, ulipokelea ndani? Hapana…je kushoot kanisani ni sisi wa kwanza? hapana! Kuna wengine walishoot Videos na Movie tena wao walifanya kwa kulidhalilisha kabisa kanisa… Nyimbo zao Zili fungiwa??? hapana!" Amesema Diamond.

Diamond amesema kuwa masuala kama hayo ndiyo yamefanya akakataa kushiriki katika tuzo za Basata.