Harmonize aliwahi kuniomba Collabo- Stivo Simple Boy

Muhtasari

•Harmonize amesema mpango huo haukufua dafu kwa kuwa wasimamizi wake wa hapo awali walikataa kuuidhinisha.

•Takriban miaka miwili iliyopita Simple Boy alimshtumu Harmonize kwa kuiba sehemu ya wimbo wake 'Inauma'.

Stivo Simple Boy na Harmonize
Stivo Simple Boy na Harmonize
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki maarufu kutoka mtaa wa Kibera Stivo Simple Boy ameibua madai kuwa staa wa Bongo Harmonize amewahi kumuomba washirikiane kutengeneza wimbo.

Akiwa mahojiano na Mpasho, Stivo alisema Harmonize alitoa ombi hilo wakati alipotembelea kituo kimoja cha redio cha hapa nchini.

Msanii huyo hata hivyo amesema mpango huo haukufua dafu kwa kuwa wasimamizi wake wa hapo awali walikataa kuuidhinisha.

"Harmonize alitaka kuongea nami kwa redio. Alitaka tupange vile mambo yatakuwa lakini wasimamizi wakakataa wakasema tutapanga hayo. Haikuwahi kufanyika," Stivo alisema.

Simple Boy aliweka wazi kuwa kutofanyika kwa collabo yake na bosi huyo wa Kondegang haukuwa uamuzi wake.

Harmonize alifanya ziara ya kimuziki nchini Kenya takriban wiki mbili zilizopita na kutumbuiza katika maeneo mbalimbali.

Nyota huyo wa Bongo na Simple Boy walikwaa jukwaa moja katika kilabu kimoja cha Nairobi ambako walikuwa wamealikwa.

Stivo amesema kuwa hakuweza kushiriki mazungumzo yoyote na Harmonize kwa kuwa kulizuka vita katika kilabu hicho.

"Ilikuwa mzuka mpaka Harmonize akashangaa. Hatukuongea. Kulitokea vita. Sijui mahali ilitokea. Mashabiki walitaka Harmonize atumbuize lakini hakutumbuiza. Mimi nilitumbuiza dakika tano tu," Stivo alisema.

Takriban miaka miwili iliyopita Simple Boy alimshtumu Harmonize kwa kuiba sehemu ya wimbo wake 'Inauma'.

Stivo alisema mwanamuziki huyo kutoka nchini jirani ya Tanzania hakuomba idhini ya kutumia kauli yake "Inauma lakini itabidi uzoee" katika wimbo wake 'Hainistui'.