Akothee azungumzia madai ya kutumia ushawishi wake kumtafutia kazi binti yake

Muhtasari

•Akothee amesema aliwafunza watoto kujisukuma wenyewe na huo ndio ustadi wa maisha wanaotumia kutafuta mafanikio.

•Akothee amemsifia sana Vesha kwa hatua kubwa ambazo amewahi kufanya katika juhudi za kujiboresha mwenyewe.

Akothee na bintiye Vesha Okello
Akothee na bintiye Vesha Okello
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee ameweka wazi kuwa hajawahi kutumia ushawishi wake kumtafutia kazi binti yake Vesha Okello.

Akothee amesema aliwafunza watoto kujisukuma wenyewe na huo ndio ustadi wa maisha wanaotumia kutafuta mafanikio.

"Watoto wangu ni watu wa kujisukuma wenyewe, hilo ndilo nililoweka ndani yao. Kama vile jina langu linaweza kufungua milango, niamini milango kadhaa imefungwa kwa ajili yao pia. Vile vile wameazima wapinzani na marafiki, Haina uhusiano wowote na ushawishi wakati huu ni thamani niliyo nayo hapa," Akothee alisema kupitia Instagram.

Mwanamuziki huyo alikuwa anajibu madai kuwa alitumia ushawishi wake mkubwa kutafutia Vesha kazi katika kampuni ya Unga Limited.

Amedai kuwa binti huyo wake mkubwa hata hakumfahamisha wakati alipokuwa anahudhuria mahojiano ya nafasi ya kazi anayotumikia pale. 

Akothee amemsifia sana Vesha kwa hatua kubwa ambazo amewahi kufanya katika juhudi za kujiboresha mwenyewe.

"Mimi Esther Akoth Kokeyo sijawahi kuomba kazi kwa ajili ya watoto wangu hata kwenye makampuni yangu, wananitumia posa na kuungana nami katika shughuli za kila siku za biashara zangu, kwa shauku hiyo ya kuweka alama, Vesha aliiba moyo wangu na nikampa sehemu ya kampuni yangu kama Mkurugenzi katika Akothee's Safaris," Akothee alisema.

Akothee amefichua kuwa bintiye aliamua ya kutafuta uzoefu katika makampuni mengine ya nje bali na yale yake ili kuweza kusaidia biashara zao vizuri zaidi.

Amesema Vesha aliwahi kupongezwa kama mwakilishi bora wa mauzo katika kampuni aliyofanyia kazi kutokana na kujitolea kwake.

Hapo awali Akothee alipakia video inayoonyesha akiwa amemtembelea Vesha katika ofisi za kampuni ya Unga Limited.

Wanamitandao walitoa hisia tofauti kutokana na ziara hiyo baadhi wakimpongeza bintiye huku wengine wakidai kuwa yeye ndiye aliyemtafutia kazi hiyo.