Mama hakunikumbuka mimi ni nani alipokuwa anaugua-Diana Marua

Muhtasari
  • Alisema baba yake alikuwa akimnyanyasa sana mama yake na wakati fulani mama yake aliwatelekeza na kuwaacha chini ya uangalizi wa baba yake
Diana Marua

Diana Marua, amesimulia kwa uchungu nyakati zake za mwisho akiwa na mamake. Alisema kuwa kwenye kitanda chake cha kifo mama yake hakuweza kumkumbuka yeye wala dada zake.

Kulingana na Diana, alizaliwa na kukulia katika familia isiyo na utulivu.

Alikuwa mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto watatu na baba yake alikuwa mlevi na alikuwa akiwanyanyasa wao na mama yao.

Alisema baba yake alikuwa akimnyanyasa sana mama yake na wakati fulani mama yake aliwatelekeza na kuwaacha chini ya uangalizi wa baba yake.

Diana alisema kwamba baba yake angerudi nyumbani akiwa amelewa na kumpiga yeye na dada zake wawili bila huruma kwa sababu ndogo.

Diana alipokuwa katika shule ya upili mama yake alimtembelea shuleni kwa siri bila babake kujua na hii iliendelea hadi alipomaliza elimu yake ya upili.

Kwa wakati huu alijua mama yake anaishi wapi na kwa kuwa alikuwa mkubwa zaidi alikuwa akichukua dada zake kwenda kumtembelea mama yake.

Alisema kuwa afya ya mamake ilidhoofika haraka baada ya kugundulika kuwa na kisukari.

Dawa alizopewa hazikufua dafu na kwa sababu ya ukosefu wa pesa hakupata nafasi ya kwenda hospitali nzuri.

Diana alikuwa akimtembelea kila siku nyumbani alipokuwa mgonjwa hadi alipokuwa kitandani.

Alisema kuwa afya ya mama yake ilipozidi kuwa mbaya ndivyo kumbukumbu yake ilivyozidi kuwa mbaya na anakumbuka siku chache kabla ya kifo cha mamake, alienda kumtembelea.

Alipofika alimsalimia mama yake lakini hakuweza kumtambua na aliendelea kuuliza ni nani.

"Mama yangu alikuwa amepoteza kumbukumbu na hakuweza kunikumbuka mimi au jina langu na ilikuwa ya uchungu sana." Diana alisema.

Diana alisema kuwa aliwapigia simu dada zake na mama yake hakuweza kuwatambua pia.

Alikuwa na maumivu makali sana aliporudi nyumbani na kuahidi kumtembelea siku chache baadaye.

Hata hivyo alipoenda kumuona mamake siku chache baadaye, alifahamishwa kuwa alikuwa amefariki saa moja kabla ya kuwasili kwake.