Khaby Lame sasa ndiye nyota anayefuatiliwa na watu wengi zaidi TikTok

Muhtasari

• Lame alizaliwa Senegal na familia yake ilihamia Chivasso, Italia akiwa na umri wa mwaka mmoja.

Image: PA Media

Mchekeshaji raia wa Senegal Khaby Lame ametajwa kuwa ndiye mtu mwenye wafuasi wengi zaidi wanaomfuatilia katika mtandao wa TikTok duniani.

Khaby Lame, 22, ambaye anatumia jina la @khaby.lame, amempiku Mmarekani Charli D'Amelio 18 ambaye alikuwa akishikilia nafasi ya hiyo tangu mwaka 2020.

Lame amefikisha wafuasi milioni 142.5 kwa usiku mmoja akiwa mbele ya Charli D'Amelio ambaye ana wafuasi 142.2.

Lame alizaliwa Senegal na familia yake ilihamia Chivasso, Italia akiwa na umri wa mwaka mmoja. Alifungua akaunti yake ya TikTok na kuchapisha video yake ya kwanza Machi 2020, baada ya kuachishwa kazi kiwandani siku za mwanzo za janga la COVID-19.

Vichekesho vya kijana huyu mwenye umri wa miaka 22 vimepata ufuasi mkubwa na amekuwa mmoja wa watengeneza maudhui wanaotambulika na kupendwa wa TikTok ulimwenguni.

Amejizolea umaarufu kwa aina yake ya uchekeshaji wa bila kuongea neno lolote zaidi ya ishara za usoni na lugha ya vitendo (video zake kwa kawaida hazijumuishi mazungumzo) zimeruhusu maudhui yake kuvutia ulimwenguni pote.