Akuku Danger aruhusiwa kuenda nyumbani,baada ya kupokea msaada kutoka kwa Wakenya

Muhtasari
  • Chapisho la mwisho alilotoa linaonyesha kuwa jumla ya Sh824, 000 zilikuwa zimekusanywa kupitia nambari ya malipo iliyowekwa kwa uchangishaji
Akuku Danger
Image: Radiojambo

Mchekeshaji wa Kenya Akuku Danger hatimaye ameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya wasamaria wema kumsaidia kuchangisha Sh824, 000 ili kulipa bili yake ya matibabu.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa kipindi cha Churchill alisambaza habari hizo njema kupitia ukurasa wake wa Instagram, na kufichua kuwa sasa yuko nyumbani na familia yake.

"Ninajisikia vizuri kurudi nyumbani na familia," Akuku Danger aliandika.

Mcheshi huyo ameachiliwa huru siku chache baada ya kuwaomba Wakenya wamsaidie kulipa bili yake ya hospitali iliyokuwa Sh823,000.

Chapisho la mwisho alilotoa linaonyesha kuwa jumla ya Sh824, 000 zilikuwa zimekusanywa kupitia nambari ya malipo iliyowekwa kwa uchangishaji.

“Jamani, kama ilivyo leo asubuhi tumefika 824K 👏👏👏🔥🔥🔥Matarajio yetu yamepita mbali zaidi. Bili ya malipo bado inaendelea, jisikie huru kutuma mchango wako. Asanteni sana🙏🙏🙏❤️

“Paybill 8024409 Akaunti MFUKO WA MATIBABU WA AKUKU. Kwa sasisho za safari yangu ya afya na sickle cell anemia follow @akukusmedicalfund,” mcheshi huyo alishiriki.

Mnamo Juni 21, 2022 mwigizaji Sandra Dacha aliripoti kwamba Akuku Danger alikuwa ametolewa hospitalini lakini akazuiliwa kutokana na bili ya hospitali ambayo ilikuwa inasubiriwa kufikia Sh823,000.