Kinuthia - Uvaaji wangu umetoka kwa fasheni za Diana Marua na Milly Chebby

Muhtasari

• Kinuthia aliwataja Diana Marua na Milly Chebby kuwa malkia ambao wamempa motisha ya kutaka kuvaa na kuonekana kama wao.

Diana Marua, Milly Chebby na Kelvin Kinuthia
Image: Official Kinuthia (Instagram)

Mkuza maudhui kwenye mtandao wa Instagram Kelvin Kinuthia ambaye umaarufu wake ni kutokana na hulka ya kuvaa nguo za kike kwa mara nyingine tena amewaacha wanamitandao wakizungumza baada ya kupakia picha Instagram akiwa kwenye vazi zuri la kike.

Kwenye maandishi yaliyofuatisha katika picha hiyo ambayo kando ameishikanisha na picha za mwanamuziki wa mtindo wa kufoka Diana Marua, ambaye ni mkewe mwaniaji wa ubunge Mathare, Kevin Bahati Kioko na mkuza maudhui wa YouTube Milly Chebby ambaye ni mkewe mchekeshaji Terence Creative almaarufu Papa Fred Ngamwaya, Kinuthia aliandika kwamba wawili hao ndio walimpa motisha na msukumo wa kutaka kuvaa kama wao.

Kelvin Kinuthia aliwamiminia wawili hao sifa na kuwaita kuwa vielelezo vyema katika fasheni yake ya uvaaji wa kike, kutoka mavazi hadi kujipodoa na nywele pia.

“Uvaaji wangu wa leo ulipata msukumo na motisha kutoka kwa vielelezo vyangu, malkia wawili ambao ni Diama Marua na Milly Chebby. Ahsante sana,” aliandika Kinuthia.

Malkia hao wawili waliuona ujumbe huu wa Kinuthia na kumjibu kwa kumhongera kwa kuchagua fasheni zao bila kujali jamii inamzungumzia nini yeye kama mwanaume ambaye ameamua kuchagua uvaaji wa kike.

“Ahsante sana, kwa kweli kabisa nimenyenyekea,” aliandika mwanamuziki wa kufoka Diana Marua.

“Ahsante, najihisi kuheshimika,” aliandika Milly Chebby.

Kinuthia amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa taarifa kinzani huku mpaka sasa wengi wakiwa hawajui jinsia yake halisi haswa baada ya mavazi ya kike kumkaa kisawasawa kama kurwa na doto kutokana na umbile la mwili wake wa kibongebonge hivi na vipodozi kumkubali kiulaini.

Mkuza maudhui huyomiaka michache nyuma habari zake zilienea sana kwamba amepokea nauli ya mwanaume kwa kujifanya mwanamke na kuikung’uta yote, jambo ambalo mamake juzi katika mahojiano alisema uvumi huo kwamba mwanake amekula hela ya mwanaume mwingine aliyotumiwa kama nauli karibu limsababishie shinikizo la damu.

Kinuthia vilevile amekuwa akipokea kashfa tumbi nzima kutoka kwa baadhi ya wakuza maudhui wenzake, aliyekuwa mwanahabari Andrew Kibe akiwa katika mstari wa mbele kukosoa vikali mitikasi anayoifanya Kinuthia katika majukwaa ya kidijitali.