"Ni ukweli nilikuwa napika chai kwa lebo ya Willy Paul," Klons Melody asema

Msanii huyo alitetea kitendo cha kufanya kazi za kijakazi pale Saldido na kusema ilikuwa tu kujitolea na si kushrutishwa

Muhtasari

• “Kama ni kikazi, hiyo sidhani kama nilikuwa natumika kupika chai, hapana. Hata si mimi peke yangu, kuna watu tu bado walikuwa wanafanya" - Klons Melody

Msanii wa kizazi kipya, Klons Melody
Image: Nicholas Kioko (YouTube screenshot)

Aliyekuwa msanii katika rekodi lebo ya Saldido International inayoongozwa na Willy Paul, Klons Melody amesema ya moyoni kuhusu jinsi ambavyo alikuwa anatumika pale Saldido na kusema sababu zake za kujiondoa na kuwa msanii huru.

Katika mahojiano ya kipekee na mkuza maudhui wa YouTube Nicholas Kioko, Melody alisema kwamba kikubwa kilichomtoa Saldido ni kutaka kukua zaidi kimuziki kwa sababu mambo yake kule yalikuwa yanachelewa sana kuenda kwa kasi aliyokuwa anaitaka kama msanii.

Melody alisema kwamba alipoingia Saldido, alifanya muziki wake wa kwanza ila akalazimika kusubiri zaidi ya miaka mitatu kabla ya muziki huo wake kuruhusiwa kutoka na kisha baadae kukaa kama miezi kadhaa kabla ya muziki wake kutoka, mradi ambao alimshirikisha bosi wake Willy Paul na baadae tena akashirikishwa kwenye Atoti na Willy Paul na mwanamuziki wa Ohangla, Musa Jakadala.

Akitolea mfano upana huu wa muda ambao ilikuwa inachukua rekodi lebo ya Saldido kuachia kazi zake, aliona kwamba kasi hiyo haimpendezi na kutaka kutafuta changamoto zaidi nje ya Saldido ili kukua zaidi na kwa kasi kimuziki.

Akizungumzia madai ya kutumika pale kama kijakasi, Melody alisema kwamba ni kweli alikuwa anatumika kupika chai na kuosha vyombo miongoni mwa kazi zingine za kijakazi ila akasisitiza kwamba alikuwa anafanya hivo kutokana na mazingira aliyolelewa kwamba lazima uhakikishe sehemu ulipo imetakata kwa kila namna.

“Ulikuwa unatumikaje pale Saldido kwa sababu nilishawahi kuambiwa kwamba ulikuwa unapikia bosi chai, ulikuwa unafanya vitu vitu pale ndani, ni ukweli ama uongo?” aliuliza Kioko.

“Ni ukweli lakini mimi unajua kulingana venye nimelelewa, nimekua nikijua kwamba ni lazima unaacha sehemu vizuri kuliko vile uliipata. Kuna vitu vingine ukiona havifanywi, unafanya tu mradi mazingira ya kazi yatakate. Kama swali ni kama nilikuwa nafanya, ni ukweli nilikuwa nafanya,” alijibu Melody.

Msanii huyo alikanusha madai kwamba kufanya hivyo hakuwa anatumika bali alikuwa anatoa huduma tu ili kufanya mazingira ya kazi kuwa safi.

“Kama ni kikazi, hiyo sidhani kama nilikuwa natumika kupika chai, hapana. Hata si mimi peke yangu, kuna watu tu bado walikuwa wanafanya lakini mimi najua nilikuwa nafanya kupika chai,” alisema Melody.