"Wewe ni mkarimu, mrembo na mwanga safi!" Michelle Ntalami amwambia Amina Rabar

Michelle Ntalami alimsherehekea Amina Rabar kwa ujumbe maalum siku yake ya kuzaliwa

Muhtasari

• "Wewe ni mwema sana. Asante kwa kuwa rafiki mzuri sana jamani." Alijibu Amina Rabar

Mtangazaji Amina Abdi Rabar na Michelle Ntalami
Image: Michelle Ntalami (Instagram)

Mjasiriamali wa vipodozi Michelle Ntalami amemsherehekea mtangazaji wa runinga Amina Abdi Rabar kwa kumuandikia ujumbe maalum na murua kabisa katika siku yake ya kuzaliwa.

Ntalami ambaye ni Rafiki mkubwa tena wa karibu kwa muda mrefu wa mtangazaji huyo mrembo ametumia ukurasa wake wa Instagram kumumiminia sifa tele la kumvisha koja la maua mazuri ya waridi Rabar huku akimtaja kuwa mtu mzuri, mnyenyekevu na ambaye hana mazoea ya kuangusha watu kirahisi.

Ntalami alifichua kwamba Rabar hapendi kusherehekea siku yake ya kuzaliwa lakini akamuomba ampe ruhusa ya kuisherehekea kwa niaba yake huku akimsherehekea kwa urafiki wao usiokuwa na doa.

“Amina, najua hupendi kusherehekea siku hii sana lakini NITAFURAHI kwa niaba yako! Wewe ni kitendawili ni wachache tu wanaoweza kufahamu. Huwaruhusu watu kuingia katika anga za urafiki wako kwa urahisi, lakini unapofanya hivyo, linakuwa jambo zuri katika ubinafsi wako halisi, na inapendeza sana kuona hivyo!” aliandika Ntalami.

Mjasiriamali huyo alizidi mbele kutema lulu kwamba Amina Rabar ni mtu ambaye wanapenda kuchezea sana huku akizungumza mambo ambayo hayatarajiwi na katika mazingira ambayo hayatarajiwi kabisa. Pia amesema Rabar ni mtu mwenye hisia za haraka kuhisi jinsi ambavyo watu wanaomzunguka wanahisi.

“Tunacheza sana! Unasema mambo yasiyofaa zaidi kwa nyakati zisizofaa zaidi. Naendelea kukuambia, Mungu akufundishe kunyamaza! Wakati huo huo, una hisia za haraka kwa jinsi watu wanavyohisi. Wewe ni mkarimu na mwenye huruma. Wewe ni mrembo. Wewe ni mwanga safi! Acha ulimwengu huu usijaribu kukushawishi vinginevyo.” Aliandika Ntalami.

Ujumbe huu ulimgusa panapofaa Rabar ambaye aliupokea kwa mikono yote miwili na kuahidi kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa njia bora zaidi siku za mbeleni.

“Aaaaaaaaa! Nitajaribu kusherehekea siku vizuri zaidi katika siku zijazo. Wewe ni mwema sana. Asante kwa kuwa rafiki mzuri sana jamani. Wewe ni gem adimu sana. Nipigie tena tunamalizia Muchene wetu. Heri ya kuzaliwa kwangu." Alijibu Amina Abdi Rabar.

Ntalami aligonga vichwa vya habari mwaka jana baada ya kusemekana kwamba alikuwa katika mahusiano ya kimapenzi na mtangazaji wa kike Makena Njeri.