Ringtone: Nimeacha kuimba muziki wa injili!

Msanii huyo mwenye utata alitangaza hivo na kuahidi kutoa sababu za maamuzi yake baadae.

Muhtasari

• Ringtone amekuwa kwa muda mrefu akijihusisha na utata mwingi huku akidai ni moja kati ya mbinu zake za kuhubiri injili.

• Alijibatiza cheo cha kuwa mwenyekiti wa wasanii wa injili nchini huku akidai ndiye msanii tajiri kuliko wote.

Msanii wa injili
Ringtone Apoko Msanii wa injili
Image: Instagram

Msanii maarufu wa injili Ringtone Apoko ameweka wqazi kwamba huenda hivi karibuni akabwaga manyanga katika suala zima la kuimba muziki wa injili.

Akiandika kwenye Instagram yake Jumatatu jioni, msanii huyo anayezungukwa na utata mwingi aliachia maneno yanayoashiria kwamba ameacha au huenda ataacha kuimba muziki wa injili.

Kama kawaida yake, Ringtone kwa lugha yake ya kizungu iliyobanangwa, aliwaomba radhi mashabiki na wafuasi wake na kuwaambia wakae ange kwani atatoa sababu za maamuzi yake Jumanne.

“Nimeacha kuimba muziki wa injili sasa. Samahani kwa mashabiki wangu ila nitapakia sababu ya maamuzi yangu kesho,” ujumbe huo wa Ringtone ulisema.

Hifahamiki kama ni kweli Ringtone ameacha kuimba na kumtukuza Mungu kupitia nyimbo na sasa kila mtu anasubiria Jumanne kama huyo msanii atatoa sababu kweli kwa sababu kwenye ujumbe wake huo, Ringtone alitagi majarida yote ya umbea humu nchini.

Sanii huyo aliyejizolea umaarufu kutokana na utata wake wa kujigamba kwa mikogo kwamba yeye ndiye msanii pekee wa injili aliye na utajiri mkubwa, mpaka kujilinganisha na wasanii wa nyimbo za dunia, kina Diamond, alisema kwamba hata mfalme huyo wa bongo fleva hamfikii katika utajiri, yaani kama kunukia basi yeye ananukia utajiri vibaya mno.

Wiki jana Ringtone alizua kioja katika mahakama alipokuwa akitoa Ushahidi na kueleza jinsi mwanablogu Robert Alai alivyomshambulia kwa rungu la Kimaasai na kumjeruhi vibaya kichwani.

Katika video iliyo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Apoko anaonekana akilia kwac kwikwi huku akisema kwamba mwanablogu huyo alipasua kioo cha gari lake la kifahari kwa rungu kabla ya kumfikia ndani na kumjeruhi kichwa.

Alai na Ringtone walijipata katika mfarakano hio mwishoni mwa mwaka jana katika tukio ambalo lilihusisha ajali ya magari yao mawili kwenye mtaa mmoja wa kifahari jijini Nairobi.

Kila mtu sasa anasubiria kuona kama kweli mwenyekiti wa injili, kama anavyojiita mwenyewe ataachia ngazi cheo hicho baada ya kutangaza kwamba ameachana na miziki ya injili.