(Video) "Nilizaa mtoto wangu bila kufanya tendo la ndoa," Msanii Malkia Karen afunguka, ilikuwaje?

Msanii Malkia Karen alisema alichukuwa hatua hiyo baada ya kukosa mwanaume wa kuzaa na yeye.

Muhtasari

• Msanii huyo alielezea kwamba alipofika wakati wa uhitaji wa mtoto, alishindwa kupata mwanaume wa kuzaa na yeye.

• Hapo ndipo alichukua hatua mbadala ya kupata ujauzito na kuzaa mtot bila kushiriki ngono.

Mwanamuziki wa Bongo Fleva Malkia Karen ambaye ni mwanawe mtangazaji maarufu nchini humo ameacha wengi vinywa wazi baada ya kudai kwambaalipata mtoto wake pasi na kushiriki tendo la ndoa na mwanaume yeyote.

Mwanamuziki huyo alikuwa akizungumza katika hafla moja aliyokuwa akizinduliwa yeye pamoja na mwanawe kama balozi wa duka la kuuza nguo na bidhaa zingine zinazotumiwa na watoto wachanga kwa jina la Josice Store.

Alisema kwamba amekuwa akiulizwa swali hilo mara kwa mara, watu na mashabiki wa kazi zake za muziki wakitaka kujua baba mtoto wake yuko wapi na ndio maana akaona ni wakati sasa wa kuweka kila kitu wazi.

“Hili suala nadhani nilikuwa nataka nilijibu, ni swali ambalo linaniandama kila siku baba mtoto yuko wapi baab mtoto yuko wapi. Ni kwamba nilipofikia wakati kwamba nina uhitaji wa kupata mtoto, sikuweza kuwa na mwenza, yaani sikupata mwanaume ambaye ninaweza nikasema huyu ni wa kwangu, tukazae labda mtoto wetu,” Malkia Karen alianza kutoa maelezo kwa maskio ya watu yaliyotegwa ndi kusikia huu muujiza wa mtoto bila tendo la ndoa.

Alielezea kwamba hospitali nyingi tu zina mbegu za wanaume zilizohifadhiwa vizuri na ambapo mwanamke yeyote mwenye uhitaji wa mtoto pasi na kutaka ngono basi anaenda kule na kuwekea na hapo anapata ujauzito.

“Nilichokifanya nilienda hospitali na nikafanya insemination, kuchukua mbegu za kiume na kuziweka kwenye mbegu zako za kike, ni kitu rahisi tu kama dakika tano na kila kitu kinaenda sawa,” alielezea Malkia Karen.

Msanii huyo alizidi kutetea hatua yake hiyo na kusema kwamba wakati mwingine inafikia hatua mwanamke unakuwa unataka mtoto lakini huhitaji kabisa kuwa na mwanaume na kusema hilo ndilo suluhu.

Alisema kwamba mbegu za wanaume zimetolewa na zipo katika hospitali mbalimbali ambapo mtu anafuata taratibu za kisheria ili kupata huduma za aina hiyo.

Malkia Karen ni mwanawe mtangazaji Garder J Habashi ambaye kwa kipindi kimoja aliwahi kuwa mpenzi wa msanii mkongwe wa bongo fleva, Lady Jaydee.