"Mko na chuki na mnaishi kwa nyumba za wazazi wenu" Thee Pluto awajia juu wenye chuki mitandaoni

Pluto amewakosoa wanaomtaka ajenge kwanza kabla ya kumiliki magari.

Muhtasari

• Aliwataka watu kuchukua mafanikio ya wenzao kama changamoto ili pia kupata baraka za kufanikiwa.

Mkuza maudhui Thee Pluto
Mkuza maudhui Thee Pluto
Image: Instagram

Mkuza maudhui maarufu nchini Thee Pluto amewachomolea makavu wale watu wanaopenda kuingilia maisha ya wasanii na watu maarufu kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Nicholas Kioko, Pluto alisema kwamba alipopakia kwenye Instagram yake kwamba anaanza biashara ya kukodisha na kuuza magari ambapo pia alipakia gari lake jingine, watu walimwagika pale na chuki na kuanza kumshauri ajenge kwanza.

Pluto aliwakosoa vikali huku akisema kwamba mtu hufai kuambia mtu kitu anafaa kufanya hata bila kujua kama kweli hicho kitu unamwambia afanye hajafanya.

“Unaniambia jenga nyumba kwanza nani anakuambia sijajenga, unajua wakati mwingine hawa watu wanachukia sana na pengine wanaishi chini ya paa za wazazi wao. Si poa, wakati mwingine chukulia vitu vingine  kama changamoto, wahongere wale walioko mbele yako ndio hata Mungu anaweza pia kukubariki,” Pluto alitema ushauri wa kiutu uzima kabisa.

Alisema kwamab yeye mafanikio yake ni kutokana na kwamba hana chuki na vijana wenzake ambao akiona wamefanikiwa anakuwa wa kwanza kuwafikia na kuwapa hongera yao.

Mkuza huyo alipata umaarufu mkubwa kutokana na mitikasi yake aliyokuwa akiifanya kwenye mtandao wa YouTube almaarufu Loyalty Test na ile ingine ya Sanitization.

Kando na kuanzisha biashara ya kukodisha na kuuza magari, Pluto pia alifichua kwamba ako na biashara kadhaa jijini Mombasa za kujenga nyumba na kukodisha vyumba vya kisasa, kwa kimombo AirBnB.

Pluto amekuwa akitupiwa maneno na baadhi ya wanamitandao wanaomsimanga kwamba anamiliki magari bila hata kujenga, baada ya kupakia picha moja akiwa na gari jeupe aina ya Prado TX ambalo alisema alizawadiwa na mwanasiasa mmoja aliyekuwa analenga kuwania uwakilishi wa kike kaunti ya Nairobi.