Ringtone: Nitakuwa naitwa Bringtone, nitavaa macheni makubwa kama OG mnoma

Ringtone ametangaza kubadilisha jina akiwa katika sanaa ya sekula.

Muhtasari

• "Mashabiki wa injili msinifuate kwa sababu mimi sikuwaita kwa Mungu, msinifuate,” - Ringtone.

Msanii Ringtone Apoko
Msanii Ringtone Apoko
Image: Instagram

Msanii Ringtone baada ya kutangaza kwamba amebwaga manyanga katika suala zima la kujihusisha na miziki ya injili, sasa ametangaza kwamba atabadilisha jina lake kutoka Ringtone hadi Bringtone.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini, Ringtone alisema kwamba rasmi ameingia kwenye tasnia ya waimbaji wa miziki ya kidunia na kuahidi kwamba atajirekebisha kitabia na pia kuwataka mashabiki wake wa injili kutomfuata na badala yake kubaki kule kwenye injili ili kuwasapoti wasanii aliowaacha kama mayatima bila mwenyekiti.

“Mimi nitakuwa ninaimba nyimbo za kidunia kwa sababu nitakuwa na tabia nzuri kwa sababu mimi sijui kufanya tabia mbaya, halafu mashabiki wa injili msinifuate kwa sababu mimi sikuwaita kwa Mungu, msinifuate,” alisema Ringtone.

“Jina la Ringtone litabaki lakini sasa nitaanza kujiita Bringtone na nitaanza kuvaa macheni makubwa makubwa, yaani nataka nikuwe OG mnoma lakini niko na tabia nzuri kwa sababu sijaacha Mungu,” aliongeza Ringtone.

Pia aliwatoa wasiwasi mashabiki wake wapya huku akisema kwamba si vibaya kujaribu na watu wasisite kumwambia ukweli wiki kesho atakapoachia kibao chake cha kwanza kaam msanii wa miziki ya kidunia.

Ringtone wiki hii iliyopita alitangaza kwamba ameacha muziki wa injili baada ya miaka zaidi ya kumi na mitano kama msanii wa kuhubiri injili kwa kile alisema kwamba ni kutokana na wanadada wengi kumsumbua.

Alitangaza nia yake kuu katika kuingia miziki ya kidunia ni kumng’oa na kumtokomeza kabisa msanii wa bongo fleva, Diamond Platnumz katika mawimbi ya humu nchini, jambo ambalo alidai wasanii kama kina Otile Brown wameshindwa kufanya kwa miaka sasa huku miziki ya nje ikizidi kuteka anga na ya wasanii wa nyumbani ikizidi kuzama bila kusikika popote.