“Zitakuwa madukani hivi karibuni" Stevo Simple Boy kuanza biashara ya sharubati

Msanii huyo alianzisha kauli hiyo ya Freshi Barida wakati ameachia kibao chake chenye jina hilo baada ya kutoka pwani.

Muhtasari

• Msanii huyo kutoka Kibera amekuwa akipiga hatua ambapo awali alianzisha kuuza sweta zenye maneno 'Freshi Barida'.

Msanii kutika Kibera, Stevo imple Boy
Msanii kutika Kibera, Stevo imple Boy
Image: Instagram

Mwanamuziki wa kizazi kipya Stivo Simple Boy aanzidi kukwea kwenye ukwasi kupitia muziki. Hii ni baada ya kutangaza kwamba hivi karibuni atazindua kampuni yake ya kutengeneza sharubati na kuita kinywaji hicho kwa jina la ‘Freshi Barida’

Akiandika kupitia Instagram yake, Simple Boy alidokeza kwamba hivi karibuni Mungu akimjaalia kinywaji hicho kitakuwa madukani.

“Na Mungu akituzidia zitakuwa madukani hivi karibuni tukuwe freshi barida,” aliandika staa huyo aliyetamba na kutambulika na wengi kwa wimbo wake wa kwanza wa ‘Mihadarati’

Staa huyo kutokea mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi alipozuka katika fani ya muziki mnamo mwaka 2019, wengi waligeuka umbile na muonekano wake kuwa kioja cha kuchekesha, wengine kumuona kama kinyago ila hakufa moyo na masimango hayo ya mitandaoni, bali alitia nta kwenye masikio na kuzidi kuchapa kazi kwa jitihada kubwa.

Aidha mwaka huu haujamwanzia vizuri baada ya kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy katika njia ya kuchafuana mitandaoni kwa cheche za nguoni huku Simple Boy akimtaja kuwa alikuwa mchepuko mwenye zaidi ya wanawake 50.

Msanii huyo pia alisemekana kudhulumiwa na usimamizi wa awali wa kazi zake za muziki ambapo uvumi ulizuka pia kwamba hadi akaunti zake za mitandaoni zilizamishwa na usimamizi huo ambapo aliamua kuanza upya.

Licha ya changamoto zote hizo, Simple Boy bado alizidi kung’ara ambapo aliachia kibao chake kwa jina ‘Freshi Barida’ na kuteka anga nchini pakubwa, mafanikio yaliyompa motisha ya kuanza kuuza sweta zenye nembo hiyo ya ‘freshi barida’

Wiki jana pia alitoa ‘remix’ ya ngoma hiyo ambayo safari hii aliwashirikisha mastaa wa gengetone kama vile Mejja, Exray miongoni mwa wengine, ngoma ambapo chini ya siku nne imefanya vizuri mno kwenye mtandao wa YouTube.