Fahamu kwa nini King Kaka alimrejesha rapa Kanambo Dede shuleni

Kanambo aliripoti katika shule yake mpya Jumanne na ataendeleza masomo kutoka alikoachia.

Muhtasari

•Kanambo alikatiza masomo yake mwaka wa 2019 wakati akiwa katika kidato cha pili baada ya kupachikwa ujauzito.

•Nana Owiti alisema hatua ya Kanambo kurudi shuleni ilimsisimua sana nusura abubujikwe na machozi.

King Kaka, Kanambo Dede na Nana Owiti
Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Rapa chipukizi Kanambo Dede hatimaye amerejea katika shule ya upili kwa ajili ya kukamilisha masomo yake.

Kanambo ambaye alijizolea umaarufu mkubwa mapema mwaka huu aliripoti katika shule yake mpya Jumanne na ataendeleza masomo kutoka alikoachia.

Bosi wa Kaka Empire, King Kaka ndiye aliyefichua habari hizo na kuweka wazi  kuwa hayo ni matakwa ya mama huyo wa mtoto mmoja.

"Alitamani, ilifanyika leo. Kanambo Dede amerudi shuleni," King Kaka alitangaza Jumanne kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake, mkewe Nana Owiti na msanii huyo wake ambaye alikuwa amevalia sare ya shule.

Nana Owiti alisema hatua ya Kanambo kurudi shuleni ilimsisimua sana nusura abubujikwe na machozi.

Alifichua kuwa yeye na mumewe walienda kumtafutia Kanambo shule nzuri baada ya kuwaambia kuwa anataka kukamilisha masomo yake.

"Moja ya matukio makubwa zaidi yalifanyika leo, @quinchermkanambo alitaka nafasi ya pili shuleni. Mara akauliza, nilimuuliza kama yuko tayari kukata dreadi zake ili tu nione mahali kichwa chake kilipo na akajibu mara moja kwa uthibitisho. Tumekuwa tukimtafutia shule nzuri yeye binafsi ( King Kaka na mimi) Kwa ufupi, amejiunga na shule leo na nilihisi kulia 😢, " Bi Owiti alisema kupitia Instagram.

Katika ujumbe wake mtangazaji pia  aliwasihi Wakenya kuziunga mkono ndoto za Kanambo kwa njia yoyote ile.

Kanambo alikuja kutambulika miezi kadhaa iliyopita baada ya video zilizoonyesha akifoka mistari kali kuenezwa mitandaoni.

Baada ya video hizo kusambaa mitandaoni kwa siku kadhaa, King Kaka alimtafuta malkia huyo na kuahidi kuinua taaluma yake ya muziki. Mwezi Januari Kanambo allijiunga na Kaka Empire na kurekodi wimbo wake wa kwanza.

"Wanawake kwa wanaume, Mkali ni @quinchermkanambo na ametoka kurekodi wimbo wake wa kwanza," Kaka alitangaza baada ya kumsajili rapa huyo kwenye lebo yake.

Kanambo alikatiza masomo yake mwaka wa 2019 wakati akiwa katika kidato cha pili baada ya kupachikwa ujauzito.

Kwa kawaida huwa hapendi kumzungumzia baby daddy wake ambaye tayari aliweka wazi kuwa huwa hasaidii kulea mtoto wao.

"Niliacha kidato cha kwanza. Hiyo ilikuwa mwaka wa 2019. Mimba ilipokua niligundua yule jamaa hakuwa akinisaidia. Sikuweza kumudu milo yangu; baada ya miezi saba migumu, nilirudi nyumbani,” Alisema katika mahojiano ya awali na Pulse.