Nandy: Labda ni mapacha! hawatakuwa kwenye mitandao, hamtajua jina, jinsia, sura

Muhtasari

• Msanii Nandy alisema mtoto atakayemzaa kamwe hatokuwa kwenye mitandao ya kijamii wala jinsia yake kujulishwa mashabiki, hata jina.

• Pia alidokeza kwamab huenda ni mapacha kutokana na vile alivyokuwa mdhaifu kwa hali yaujauzito.

Msanii Nandy
Msanii Nandy
Image: Maktaba, Instagram

Malkia wa Bongo Fleva Nandy amefichua makubaliano na mumewe Billnass kuhusu malezi ya mtoto wao ambao wanamtarajia baada ya kuweka wazi taarifa na dhibitisho la ujauzito wiki jana.

Akizungumza katika hafla ya kuzungumzia tafrija ya hserehe zake za kila mwaka almaarufu Nandy Festival ya mwaka huu wa 2022, nandy alisema kwamba maelewano yao yapo kwamba hakuna kutaja jina la mtoto wala kuonesha sura yake na hata kumfungulia akaunti za mitandaoni kama ambavyo wanajaribu kufanya wengi wa watu mashuhuri kwa watoto wao.

“Sidhani kama tutaliweka wazi jina la mtoto wala sidhani kama tutakuja kutoa jinsia yake au hata kuwa na ukurasa wake wa Instagram wala kuonekana hata kidogo mitandaoni,” alisema Nandy.

Msanii huyo alisema kwamba hayo ndio maelewano Madhubuti ambayo wameyaratibu ili kwamba wampee mtoto nafasi akue mwenyewe akishafikisha umri wa kujielewa basi akajifanyie mambo hayo mwenyewe.

“Ni makubaliano na baba mtoto tumependelea hivo tumpe nafasi ya kua kama yeye akishakuwa mkubwa ataamua kuwa nani na sio sisi tumuamulie kuanzia akiwa mdogo. Suala la mtoto nadhani tumelimaliza kwamba hatokuwa kwenye mitandso ya kijamii, hakuna mtu atajua jinsia wala jina,” Nandy alisema.

Msanii huyo akijibu maswali ya wanahabari waliokusanyika katika ukumbi huo, mmoja alitaka kubaini kama kweli ni mtoto au watoto akiwa na maana kama ni mapacha, na Nandy alisita kidogo na kusema hata yeye hajui lakini pia akakataa kupuuzilia mbali uwezekano na kuwapo kwa mapacha.

“Sijui, labda ni mapacha kweli, si mnaona tu kama nilivyodhaifu, labda ni mapacha kiukweli lakini nisingependa sana kumuweka au kumzungumzia mtoto labda yuko, hivi anaitwa nani, atafanya nini, hapana kiukweli,” Nandy alidokeza uwezekano wa kutarajia mapacha.