Mmiliki wa Facebook, Zuckerberg aonesha magari ya kitambo wanayotumia na mkewe

Tajiri huyo alipakia magari hayo ya kitambo na kuzua mjadala mitandaoni kwani wengi walitarajia anatumia magari ya kisasa.

Muhtasari

• Mark Zuckerberg ambaye ni tajiri mmiliki wa Facebook alizua mjadala Facebook baada ya kupakia magari makuukuu ya zamani na kusema kwamba ndio wanatumia yeye na mkewe.

Magari ya mmiliki wa Facebook na mkewe
Magari ya mmiliki wa Facebook na mkewe
Image: Facebook///Mark Zuckerberg

Mmiliki wa mtandao mkubwa zaidi, Facebook Mark Zuckerberg amewaacha wengi wakizungumza baada ya kupakia picha inayoonyesha magari mawili ya kitambo ambayo alisema ni yake na ya mke wake.

Picha hiyo iliwashushua watumiaji wengi wa mtandso huo ambao walishangaa ni kwa nini mtu anayenukia utajiri kama Zuckerberg anaweza miliki gari la kitambao hali ya kuwa watu wa kawaida tu wakipata cheo kidogo wanatanua vifua na kutamba mpaka kutafuta magari mengine ya kifahari kama sehemu ya msafara wao popote waendapo.

“Kwa nini wewe na Elon Musk mnaishi maisha rahisi. Je! mnajifanya au vipi? Sipendi jinsi nyinyi mnavyocheza na hisia zetu,” mmoja aliandika akihisi Tajiri huyo anacheza shere na hisia za watu kwani kwa kufikiria kwa kawaida si rahisi upate mtu Tajiri anamiliki gari la miaka ya 80 kama hayo aliyopakia Zuckerberg na kusema ni yake na ya mke wake.

Mark Zuckerberg kwenye picha hiyo aliandika “ Yake na yangu” akimaaisha yeye wa jinsia ya kike ambaye bila shaka ni mkewe na yeye mwenyewe.

Wakenya wengi waliofurika kwenye sehemu ya kuachia maoni waliachia kila aina ya utani huku wakiwasuta baadhi ya wanasiasa wa humu nchini ambao pindi tu baada ya kuingia bungeni na uongozini wanaanza kutafuta magari ya kifahari na hata kuweka vioo vyeusi ili kukwepa kuonana uso kwa uso na wananchi waliowapigia kura.

Baadhi waliwataka viongozi kusoma kutoka kwa Zuckerberg ambaye ni Tajiri mkubwa lakini bado kutokana na magari yale basi ni wazi kwamba hata maisha yake ni ya kawaida tu, kinyume na wengi wanavyomfikiria kutokana na kujua kwamba mmiliki huyo wa Facebook ndiye mtu wa kwanza kuanzisha jukwaa hilo la mtandaoni ambalo mpaka sasa linaongoza wa watu wanaolitumia na hivyo kumlimbikizia mabilioni ya pesa katika kila sekunde iendayo kwa Mungu.

Wengine walisema wamepata funzo kutoka kwa hizo picha na kuhisi kuhimizika kwamba kweli furaha ya maisha haitokani na kumiliki mali yenye thamani iliyotukuka bali ni kuwa na amani maishani na hicho ndicho kitu cha muhimu.